Mkutano mkuu wa 3 wa kamati kuu ya 17 ya chama cha kikomunisti cha China ulipitisha na kutangaza waraka muhimu unaolenga kusukuma mbele mageuzi ya vijijini, na kuamua wazi na rasmi sera ya kuwaruhusu wakulima kupanga mpango halali wa matumizi ya ardhi walizokodishwa kwa mkataba. Wataalamu husika wanaona kuwa, hatua hiyo inasaidia kupanua ukubwa wa uzalishaji wa kilimo vijijini, kubana matumizi ya ardhi, na kuinua ufanisi wa maendeleo ya uchumi wa vijijini.
Mkutano mkuu wa 3 wa kamati kuu ya 17 ya chama cha kikomunisti cha China uliofungwa mwezi Oktoba ulitoa mpango wa kumwezesha kila mkulima aongeze mapato kwa mara mbili ifikapo mwaka 2020. Kuanzisha soko la kuwasaidia wakulima wakodishe mashamba, kuwaruhusu wakulima kuendeleza uzalishaji wa kilimo kwa ukubwa wa kufaa kutahakikisha utimizaji wa mpango huo.
China haitekelezi utaratibu wa kubinafsisha ardhi. Watu wana haki ya kutumia ardhi badala ya kumiliki ardhi. Kwa mujibu wa utaratibu wa kutumia ardhi kwa mkataba kwa kila familia ya wakulima vijijini ulioanza kutekelezwa katika mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, wakulima wanaweza kutumia ardhi ndogondogo kwa muda mrefu baada ya kusaini mkataba. Kuanzishwa kwa utaratibu huo kuliwahamasisha wakulima wa China washughulikie uzalishaji, na kumetoa mchango mkubwa katika kuhakikisha uzalishaji wa kilimo na usalama wa vyakula, na kuongeza mapato ya wakulima. Lakini kutokana na kuinua kwa uwezo wa uzalishaji na kuenea kwa matumizi ya sayansi na teknolojia, vijiji vya China vinakabiliwa na tatizo la mashamba madogomadogo ambalo limepungua ufanisi wa matumizi ya ardhi.
Ofisa anayeshughulikia kazi ya kilimo wa kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China Bw. Chen Xiwen alisema,
"Kwa mfano, kwa baadhi ya familia, watoto wao wameondoka na kwenda sehemu nyingine, wazee wanaobaki hawana uwezo wa kufanya kazi mashambani, au baadhi ya wakulima wanafanya kazi za vibarua mijini, hawataki kushughulikia uzalishaji wa kilimo tena. Kutokana na hali hizo, katika siku zilizopita China ilitunga sheria na sera ikiamua kuwa wakulima wanaweza kukodisha mashamba waliyokodishwa kwa mkataba."
Ingawa China imeamua kuwa wakulima wanaweza kukodisha mashamba kwa mkataba, lakini kutokana na ukosefu wa utaratibu na kanuni husika, uamuzi huo haufanyi kazi vijijini. Na mkutano mkuu wa 3 wa kamati kuu ya 17 ya chama cha kikomunisti cha China uliamua wazi kuwa wakulima wanaruhusiwa kupanga mpango wa matumizi ya ardhi kwa njia ya kuhamisha, uendeshaji, kukodisha na kushughulikia uzalishaji kwa ushirikiano wa kihisa, na kuendeleza uzalishaji wa kilimo kwa ukubwa wa kufaa. Mtafiti wa taasisi ya utafiti wa uchumi wa vijijini wa wizara ya kilimo ya China Bw. Zhao Yutian anaona kuwa hatua hiyo itasukuma mbele uchumi wa vijijini, akisema,
"Uamuzi huo utatoa mchango kwa pande mbili. Kwanza, uamuzi huo utatoa uungaji mkono wa kisera kwa kuanzisha utaratibu wa kupanga mpango wa matumzi ya ardhi; pili uamuzi huo utainua uwezo wa uzalishaji, kuongeza matumizi ya teknolojia, kuvutia mitaji ya nchini na nchi za nje, na kuhimiza mzunguko wa mazao ya kilimo. Uamuzi huo ni muhimu sana kwa maendeleo ya vijijini na kutatua masuala yanayohusu kilimo, vijiji na wakulima."
Kijiji cha Xiaogang cha wilaya ya Fengyang mkoani Anhui ni chimbuko la utaratibu wa kutumia ardhi kwa mkataba kwa kila familia ya wakulima vijijini nchini China. mwaka 1978, wakulima wa kijiji hicho walianza kusaini mkataba wa kulima mashamba kwa familia moja moja. Na hii ilikuwa mwanzo wa mageuzi ya utaratibu wa kukodi mashamba vijijini nchini China. Hivi sasa kijiji hicho kinakusanya mashamba madogo madogo tena kupanda zabibu na uyoga, kuendeleza uzalishaji wa kilimo kwa ukubwa, kilimo chenye sifa ya kipekee, na utalii wa vijijini. Kiongozi wa kijiji hicho Bw. Shen Hao alisema,
"Sisi sote tunaona kuwa, njia ya jadi ya uzalishaji kwa familia moja moja inaweza kuhakikisha maisha ya kimsingi ya wakulima, lakini haiwezi kuwasaidia wakulima wajitajirishe. Wakulima wanatakiwa washirikiane kuanzisha njia mpya ya uzalishaji, yaani kuwaruhusu wakulima kukodisha mashamba waliokodishwa kwa mkataba, kuendeleza uzalishaji wa kilimo kwa ukubwa unaofaa na kuendeleza kilimo cha kisasa, basi watatajirika."
Katika mji wa Daye ulioko mkoani Hubei ambao ni mkoa unaozalisha nafaka kwa wingi, mkulima Hou Anjie mwenye umri wa miaka 51 alikodi mashamba zaidi ya hekta 1300 kwa kusaini mikataba na wakulima elfu 20 kutoka vijiji vinane. Kwenye mashamba hayo kuna mpunga uliokomaa wenye rangi ya dhahabu, mashine za kilimo zinazofanya kazi na malori ya kubebea nafaka. Mwaka huu mashamba yake yamepata mavuno mazuri. Bw. Hou alisema,
"Tunalima mashamba na kuvuna mazao kwa mashine. Tunapanda, kuvuna na kuuza mazao na kununua mbolea kwa pamoja, bei za mazao na gharama ya uzalishaji ni chini zaidi kuliko wale wanaolima mashamba madogo madogo."
Bw. Hou Anjie alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kabla ya uzalishaji mkubwa wa kilimo, wakulima walilima mashamba kwa familia moja moja, na mavuno ya nafaka yalikuwa kilo 4500 kwa hekta kwa mwaka. Hivi sasa akitumia teknolojia za kisasa na mashine, anapanda mazao kwenye mashamba hayo kwa pamoja, na mavuno ya nafaka yamefikia kilo 7500 kwa hekta. Hivyo wakulima wa huko wanapenda kukodisha mashamba yao. Bw. Hou alisema,
"Wakulima wanapenda kukodisha mashamba yao kwa sababu vijana wanafanya kazi za vibarua mijini, hivyo hakuna mtu anayeshughulikia uzalishaji mashambani, tena wakulima wakilima mashamba kwa familia moja moja, hawawezi kupata faida nyingi, kwa sababu bei za mbolea ya kemikali na dawa za kuulia wa dudu zote zimepanda."
Wengi kati ya wakulima zaidi ya milioni 700 wa China wanashughulikia uzalishaji wa kilimo kwenye mashamba madogo madogo, na ufanisi wa uzalishaji ni mdogo. Kuwaruhusu wakulima kukodisha mashamba waliokodishwa kwa mkataba, kutainua ufanisi wa uzalishaji wa kilimo, kuongeza mapato ya wakulima, na kuharakisha mchakato wa maendeleo ya miji nchini China.
Wataalamu walisema baada ya sera ya kuwaruhusu wakulima kukodisha mashamba kwa mkataba kutolewa, soko la kukodisha mashamba vijijini litaanzishwa haraka.
|