Hivi sasa simu za mkononi zinachukua hadhi muhimu katika maisha ya watu wa China, kiasi kwamba ni mahitaji ya kila siku. Lakini amini usiamini, miaka 30 iliyopita katika sehemu nyingi nchini China, simu ilikuwa ni bidhaa isiyo ya kawaida, wakati huo njia ya posta ilikuwa ni njia muhimu ya mawasiliano kati ya watu wanaoishi katika sehemu mbili zilizoko mbali. Katika kipindi hiki cha leo, tutamfahamu Bw. Zhang Jijun ambaye ni mkazi wa Guangzhou, mji wa kusini mwa China, naye atatuelezea kuhusu simu alizowahi kutumia katika muda wa miaka 30 iliyopita. Karibuni.
Bw. Zhang Jijun mwenye umri wa miaka 55 ni mzaliwa wa Guangzhou, mji maarufu ulioko kusini mwa China. Mji huo unapakana na mkoa wa utawala maalumu wa Hong Kong. Miaka 30 iliyopita, huduma ya mawasiliano mjini Guangzhou ilikuwa katika hali duni, ambapo simu ilikuwa bidhaa ya kawaida huko Hong Kong. Bw. Zhang akitaja mawasiliano ya wakati huo, alisema yalikuwa magumu sana. "Sisi mabaharia tulisafiri mara kwa mara. Kila tulipofika kwenye bandari ya ndani yoyote, tulitaka kuwapigia simu jamaa walioko nyumbani, tukiwaelezea tuko salama. Lakini wakati huo ilikuwa huduma ya simu haipatikani nyumbani isipokuwa ofisini, kwa hiyo ilitubidi tupige simu wakati jamaa zetu walipokuwa wakifanya kazi. Kwa upande wetu, pia tulipaswa kupiga simu katika idara ya posta na simu. Niliwahi kusubiri nusu saa kwenye idara ya posta na simu ya bandari ya Zhanjiang, ili niwapige simu jamaa zangu walioko mbali."
Huduma ya mawasiliano ya simu ilikuwa katika hali duni kabla ya China kuanza kutekeleza sera ya mageuzi na ufunguaji mlango. Takwimu zinaonesha kuwa, mwaka 1978 idara za simu kote mkoani Guangdong zilikuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa simu laki 2 tu, huku idadi hiyo huko Hong Kong ilikuwa zaidi ya milioni 1.2, wakati huo idadi ya wateja wa simu ilikuwa laki moja hivi.
Ili kuharakisha maendeleo ya huduma ya mawasiliano, mwazoni mwa miaka ya 80 ya karne iliyopita, serikali ya China ilianza kuwatoza malipo maalumu watu waliotaka kufungiwa simu nyumbani, na fedha hizo zilitumika katika ujenzi wa mtandao wa simu. Wakati huo malipo ya kufungiwa simu moja nyumbani ilikuwa zaidi ya Yuan elfu 4, lakini wastani wa mshahara wa mwezi kwa watu wa China ulikuwa Yuan 100 tu.
Kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 1995, uchumi wa mkoa wa Guangdong ulipata maendeleo ya kasi sana, ambapo kwa wastani ongezeko la uchumi lilizidi asilimia 30. Maendeleo ya uchumi yaliweka msingi imara kwa maendeleo ya huduma ya mawasiliano mkoani Guangdong. Hadi mwishoni mwa mwaka 1990, idara za simu mkoani Guangdong zilikuwa na uwezo wa kutoa huduma kwa simu milioni 1.8 na idadi ya wateja wa simu ilifikia milioni 1.13, idadi hizo mbili zote zilizidi zile za Hong Kong. Katika kipindi hiki, Bw. Zhang alifunga simu nyumbani kwake.
Alisema "Ilikuwa mwaka 1992, 93 hivi, wakati ambapo watu wengi walifunga simu nyumbani, kwa hiyo majirani waliposalimiana walipenda kuulizana: je, ulifunga simu nyumbani au yeye alifunga simu nyumbani kwake?"
Mwezi Novemba mwaka 1987 mtandao wa simu za mkononi ulianzishwa mjini Guangzhou, huu ni mtandao wa kwanza wa namna hii nchini China. Bw. Zhang akikumbusha alisema "Nilianza kutumia simu ya mkononi mwaka 1993, nilipewa simu hiyo na bosi wangu kutokana na kazi niliyofanya. Hadi mwaka 1997 mimi mwenyewe nilinunua simu ya mkononi, gharama za simu hiyo pamoja na gharama za kuchagua namba na gharama za kupata huduma kwa jumla zilikuwa Yuan elfu 10, wakati huo zilikuwa pesa nyingi sana ambazo watu wengi hawakuweza kumudu."
Baada ya mwaka 2000, idadi ya wateja wa simu ya mkononi mjini Guangzhou na hata China nzima ilianza kuongezeka haraka sana, kiasi kwamba katika miji ya China, mbali na watoto karibu kila mtu ana simu ya mkononi.
Takwimu zilizotolewa na idara ya usimamizi wa mawasiliano ya simu ya mkoa wa Guangdong zinaonesha kuwa, hadi mwezi Agosti mwaka 2008, idadi ya wateja wa simu ya mkononi mkoani Guangdong ilifikia milioni 80, na kuzidi ile ya wateja wa simu ambayo ni milioni 30. Hivi sasa simu ya mkononi ni bidhaa zinazonunuliwa kwa urahisi na watu wa kawaida badala ya bidhaa zenye thamani kubwa. Mbali na kupiga simu, watu pia wanaweza kupiga picha, kusikiliza muziki, kutembelea mtandao wa Internet na kusoma magazeti kwa kutumia simu ya mkononi. Bw. Zhang alisema "Zamani nilitumia simu ya mkononi kupiga simu tu, baadaye nilianza kuitumia kwa kutuma ujumbe, na sasa naweza kuitumia kupata huduma ya mtandao wa Internet, kutuma picha na vitu vya audio. Simu ya mkononi ya hivi sasa inatoa huduma za aina mbalimbali. Nimeagiza makala za magazeti ili nisome magazeti kwenye simu ya mkononi, ni rahisi kweli, si lazima niende kununua magazeti kila siku."
Licha ya hayo, huduma ya simu za mkononi nchini China imeanza kuingia kwenye kipindi cha tekenolojia mpya ya 3G. Imefahamika kuwa, huduma hiyo ilitolewa kwa majaribio mwezi Aprili mwaka huu nchini China. Bw. Zhang alieleza kuvutiwa na teknolojia hiyo mpya, "Niliwahi kutoa maombi ya kutumia simu inayoweza kuwaona watu kwa majaribio, lakini kwa bahati mbaya sijapewa nafasi hii. Simu zinazotumia teknolojia hiyo mpya zinatumika kwa majaribio, bado hazijaanza kuingia sokoni, kwa hiyo hatuwezi kuzitumia mpaka sasa."
Kutokana na huduma ya simu inayoendelezwa haraka, Bw. Zhang alitoa maoni yake kuwa, hakutarajia kasi kubwa ya maendeleo, na hivi sasa ana matumaini ya kutumia mawasiliano ya simu yanayotumia teknolojia za kisasa zaidi.
|