Wapiganaji 200 wa kundi la IS wauwawa na jeshi la Iraq
Jeshi la usalama la Iraq wiki hii limetwaa tena mtaa mmoja na vijiji viwili, na kuwaua wapiganaji 200 wa kundi la Islamic State baada ya askari wa jeshi hilo kuanza operesheni ya pili kuwaondoa wapiganaji wa kundi hilo kutoka Mosul.
Askari wa kupambana na ugaidi wamewashambulia wapiganaji walioko mstari wa mbele wa kundi la Islamic State kwenye mitaa kadhaa mashariki mwa Mosul, na kuamua kuudhibiti mtaa wa al-Quds wakati mapambano makali yanaendelea kwenye mtaa wa jirani.
Kwenye upande wa kaskazini, askari wa jeshi la Iraq walikomboa kijiji cha al-Sada na kijiji cha Tawiyla na kupandisha bendera ya Iraq kwenye jengo kuu baada ya kupambana vikali na wapiganaji wa kundi la Islamic State.
Wakati huo huo Rais Vladimir Putin wa Russia ametangaza kuwa Russia itapunguza jeshi lake nchini Syria, lakini itaendelea kupambana na ugaidi.
Kwa mujibu wa tovuti ya ikulu ya Russia, rais Putin alipokutana na waziri wa ulinzi Bw Sergei Shoigu na waziri wa mambo ya nje Bw Sergei Lavrov, amesema Russia itaendelea kupambana na ugaidi bila masharti, itaendelea kuiunga mkono serikali ya Syria kwenye mapambano dhidi ya ugaidi, na kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa na serikali ya Syria.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |