Wabunge wa Somalia waapishwa
Wajumbe 284 wa mabaraza mawili ya Bunge la Somalia waliapishwa wiki hii mjini Mogadishu.
Katibu wa bunge la Somalia Bw Abdikarin Haji Buh amesema wenyeviti wa mpito wameteuliwa na wataendesha kikao kijacho kitakachochagua maspika wa mabaraza mawili ya bunge hilo.
Spika wa zamani wa bunge la Somalia Bw Mohamed Osman Jawari amesema maspika wa zamani wamekabidhi madaraka kwa wenyeviti wa mpito.
Wajumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia wamepongeza hatua ya kuapishwa kwa bunge jipya la Somalia, na kuitaja kama alama ya maendeleo na umoja kwa Somalia.
Kiongozi wa Tume ya Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM Bw Francisco Madeira, amesema kuapishwa kwa wabunge wapya ni hatua muhimu kwa Somalia kufikia utulivu wa kisiasa na demokrasia, kufuatia nchi hiyo kujenga upya taasisi zake za kitaifa baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo miwili.
Hata hivyo Uchaguzi wa rais wa Somalia uliopangwa kufanyika tarehe 28 Desemba, umeahirishwa tena hadi mwezi Januari mwaka kesho, kutokana na mikwaruzano kuhusu uchaguzi wa mabaraza ya bunge.
Hii ni mara ya nne kwa uchaguzi huo kuahirishwa.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |