Sudan na Sudan Kusini zarefusha muda wa makubaliano ya kusafirisha msaada wa kibinadamu
Serikali za Sudan na Sudan Kusini zimerefusha wiki hii muda wa makubaliano ya pamoja kuhusu kuipatia Sudan Kusini msaada wa kibinadamu kwa kupitia ardhi ya Sudan kwa miezi sita zaidi.
Naibu kamishna wa ofisi ya msaada wa kibinadamu ya Sudan Bw Ahmed Mohamed Osman amesema kwamba kuongezwa muda kwa makubaliano hayo kunaweza kuimarisha uhusiano wa kibinadamu kati ya nchi hizo mbili.
Osman amesisitiza kwamba serikali ya Sudan iko tayari kushirikiana na jumuiya ya kimataifa kusaidia kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wahitaji nchini Sudan Kusini.
Makubaliano hayo yanaliwezesha Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa WFP nchini Sudan kuwapatia msaada wa chakula watu zaidi ya laki 2 walioko mkoa wa Upper Nile nchini Sudan Kusini.
Wakati huo huo Waziri wa mambo ya nje wa Sudan Kusini Deng Alor amesema, rais Salva Kiir atafanya ziara nchini Sudan katika siku chache zijazo.
Alor aliwasilisha ujumbe wa rais Kiir kwa mwenzake wa Sudan Omar al-Bashar kuhusu uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |