Vikosi maalum nchini Ivory Coast vyateka mji wa Adiake
Vikosi maalum nchini Ivory Coast vimetoka nje ya kambi yao na kufyatua risasi hewani na pia kuteka mji mmoja ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo,
Tukio hilo limeshuhudiwa katika mji wa Adiake, kilomita 95 hivi kutoka mji mkuu Abidjan, na linafanyika wakati nchi hiyo ya Afrika magharibi ikikabiliwa na msururu wa majaribio ya mapinduzi.
Wakazi wa mji huo walikimbilia usalama na kujifungia kwenye nyumba zao.
Duru zinaarifu kwamba kikosi hicho cha jeshi kinaitaka serikali kuwalipa marupurupu yao.
Jenerali Lassina Doumbia, ambaye ni kamanda wa vikosi maalum amesafiri kwenda kwenye mji huo wa Adiake kukutana na wanajeshi hao katika jaribio la kusuluhisha mzozo uliopo.
Serikali ya Ivory Coast imeanza juhudi za kujaribu kuzima mgomo wa wanajeshi wa vikosi maalumu nchini humo, wakati huu hofu ya kuenea kwa vurugu mpya ikizidi kutanda baada ya majuma kadhaa ya maandamano ya vyombo vya usalama kushinikiza nyongeza ya mshahara.
Waziri wa Habari Bruno Kone amelazimika kufanya mazungumzo na wawakilishi wa wanajeshi hao kujaribu kupata suluhu ili kunusuru kile ambacho wadadisi wa mambo wanasema ni uasi ndani ya jeshi.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |