Zimbabwe yaanza kuandikisha wapiga kura kwa mfumo wa biometric kabla ya uchaguzi wa mwaka ujao
Tume ya Uchaguzi ya Zimbabwe imeanza kuandikisha wapiga kura kwa mfumo wa biometric, ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka ujao.
Kwa mara ya kwanza Zimbabwe inatumia mfumo huo ili kupata idadi halisi ya wapiga kura, ikimaanisha kuwa hata wale waliojiandikisha awali wanatakiwa kujiandikisha upya. Zoezi la uandikishaji wapiga kura litaendelea mpaka Januari 15 mwakani.
Tume hiyo inatarajia kuandikisha wapiga kura milioni 7 kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka ujao, ikiwa ni ongezeko kutoka milioni 6.8 walioandikishwa katika uchaguzi wa mwaka 2013.
Rais wa Zimabawe Robert Mugabe na mkewe Grace, wamekuwa watu wa kwanza kujiandikisha kama wapiga kura kabla ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Rais hata hivyo alisema kuwa shughuli hiyo ya kujiandikisha ilichukua muda mrefu.
Raia wote wa Zimbabwe wakiwemo wale waliopiga kura kwenye uchaguzi uliopita, watahitaji kujiandikisha upya kwa kutumia mfumo mpya ambao unachukua alama za vidole na picha za uso.
Ni vifaa 400 kati ya 3000 vya kuwandikisha wapiga kura vilivyowasilishwa nchini humo kutoka China kwa shughuli hiyo ambayo itakamilka mwezi Januari mwaka 2018.
Tume ya uchaguzi inasema kuwa inalenga kuwaandikisha watu milioni 7.
Bwana Mugabe ambaye ameingoza nchi tangu mwaka 1980, anatarajiwa kuwa mgombea wa chama cha Zanu-PF kwenye uchaguzi huo ambao unatarajiwa kuandaliwa kati kati mwa mwaka ujao.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |