Mahakama kuu ya Iraq yaliagiza jimbo la wakurd lisimamishe upigaji kura za maoni
Mahakama kuu ya Iraq wiki hii imelitaka jimbo la wakurd lisimamishe upigaji kura za maoni uliopangwa kufanyika tarehe 25 mwezi huu.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya habari ya mahakama kuu ya Iraq imesema wajumbe wote wa mahakama kuu jana walikutana kujadili suala la upigaji kura za maoni katika jimbo la wakurd na maeneo mengine. Baada ya mkutano wao, mahakama ilitoa agizo la kusimamisha mchakato wa upigaji kura za maoni.
Mwezi Juni mwaka huu jimbo la wakurd la Iraq lilitangaza kupiga kura za maoni kuhusu kujitenga na Iraq mwezi huu, kitendo ambacho kimepingwa vikali na serikali kuu ya Iraq, Uturuki na Iran.
Aidha ofisa mwandamizi wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia sera za ki diplomasia na usalama Bibi Federica Mogherini, ametoa taarifa akipinga kupigwa kwa kura za maoni kwenye jimbo la wakurdi nchini Iraq.
Taarifa inasema Umoja wa Ulaya unasisitiza kuunga mkono umoja, mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya Iraq, na kwamba mgogoro kati ya serikali ya jimbo la wakurd na serikali kuu ya Iraq unapaswa kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo ya kiujenzi, kwenye msingi wa katiba ya Iraq.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |