Serikali ya Zimbabwe yatoa ulinzi kwa wagombea wa uchaguzi
Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amenusurika baada ya mlipuko kutokea mkutano aliokuwa anauhudhuria Bulawayo ambako watu 49 walijeruhiwa.
Video kutoka uwanja wa michezo wa White City unaonesha Bw Mnangagwa akiondoka kwenye jukwaa baada ya kutoa hotuba, mlipuko unapotokea.
Makamu wa Rais wa kwanza wa Zimbabwe Constantino Chiwenga pia alipata majeraha madogo.
Kufuatia tukio hilo serikali ya Zimbabwe imeamua kutoa ulinzi kwa wagombea wote katika uchaguzi mkuu wa tarehe 30 mwezi ujao endapo watahisi maisha yao yako hatarini.
Makamu wa rais wa nchi hiyo Constantino Chiwenga amesema hayo katika mkutano wa kampeni uliofanyika Chitungwiza, kusini mwa mji mkuu wa Zimbabwe, Harare. Amesema mlipuko wa bomu uliotokea jumamosi wakati rais Emmerson Mnangagwa alipokuwa akitoka jukwaani baada ya kumaliza mkutano wa kampeni mjini Bulawayo ulikuwa ni shambulizi la kigaidi.
Rais Mnangagwa aliingia madarakani Novemba mwaka jana baada ya kuondolewa madarakani kwa Robert Mugabe aliyekuwa ameliongoza taifa hilo kwa miaka 37.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |