Marekani yaweka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran
Rais Donald Trump wa Marekani ametangaza kuwa nchi yake inaweka vikwazo vipya na vikali zaidi dhidi ya Iran, wakati hali ya wasiwasi ikizidi kati ya nchi hizo mbili.
Rais Trump amesaini amri ya rais katika Ikulu ya Marekani ikiweka vikwazo vya ziada vya kiuchumi dhidi ya Iran, na kuwaambia wanahabari kuwa watu waliolengwa katika vikwazo vipya ni pamoja na kiongozi mkuu wa Iran Bw. Ayatollah Ali Khamenei, ofisi yake, na wengine wengi.
Habari nyingine zinasema, balozi wa Iran nchini Marekani Bw. Majid Takht Ravanchi ameilaani Marekani kuzuia ushiriki wa nchi yake katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mvutano kati ya Iran na Marekani.
Balozi huyo amesema, Iran ina haki ya kushiriki kwenye mkutano huo kutokana na eneo la anga la nchi hiyo kuvamiwa na ndege za kijasusi za Marekani zisizo na rubani.
Majid amesema vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya maofisa wa Iran, vinamaanisha kuwa Marekani inakiuka sheria za kimataifa. Uamuzi huo wa Marekani ni dalili nyingine kwamba Marekani haiheshimu sheria za kimataifa na maoni ya kimataifa.
Rais Donald Trump wa Marekani wiki hii alisaini amri ya kuweka vikwazo dhidi ya kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na ofisi yake, na wale wanaohusiana na yeye. Marekani pia imetangaza kuwa waziri wa mambo ya nje wa Iran pia amewekwa kwenye orodha ya watu watakaowekewa vikwazo baadaye.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |