Washtakiwa watatu wapatikana na hatia ya kupanga shambulizi la kigaidi Chuo Kikuu cha Garissa
Mahakama jijini Nairobi nchini Kenya, imewakuta na hatia washtakiwa watatu kati ya wanne waliokuwa wameshtakiwa kwa kosa la ugaidi, baada ya shambulizi katika Chuo kikuu cha Garissa Kaskazini mwa hiyo mwaka 2015, na kusababisha vifo vya watu karibu 150 wengi wakiwa wanafunzi.
Waliopatikana na hatia ya kufanikisha na kupanga shambulizi hilo wakishirikiana na kundi la Al Shabab ni pamoja na Mtanzania Rashid Charles Mberesero na raia wa Kenya wenye asili ya Somalia Hassan Edin na Mohamed Abdi.
Hata hivyo, mshtakiwa mwingine Sahal Diriy maarufu kama Sahali Diriye Hussein amefutiwa mashtaka ya ugaidi.
Hukumu dhidi ya watatu hao itatolewa tarehe 3 mwezi Julai. Sheria ya Kenya kuhusu ugaidi inaeleza kuwa, yeyote anayepatikana na kosa kama hili atakitumikia kufungo cha maisha jela.
Wakati kesi hiyo ikiendelea, washtakiwa wote walikanusha mashtaka 156, likiwemo lile la ugaidi.
Kundi la kigaidi la Al Shabab kutoka nchini Somalia, lilijigamba kuhusika na shambulizi hilo baya katika chuo hicho ambacho kinapakana karibu na mpaka wa Somalia.
Magaidi hao walivamia Chuo hicho wakati wanafunzi wakiwa kwenye sala ya alfajiri na kuwateka wanafunzi hao Wakiristo kwa Waislamu kwa saa zaidi ya 15 kabla ya operesheni hiyo kumalizika.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |