Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema kuwa, mazingira nchini Burundi bado hajawa mazuri kwa sasa kuwarejesha wakimbizi wanaohifadhiwa Kigoma, nchini Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na tawi la Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika la UNHCR inasema kuwa, ingawa hali ya usalama imeboreshwa kwa ujumla, lakini UNHCR inaona kuwa hali nchini Burundi haifai kwa wakimbizi kurudi.
Taarifa hiyo ilitolewa ili kujibu onyo lililotolewa na serikali ya Tanzania wiki iliyopita kwa mashirika na watu binafsi ambao wanazuia wakimbizi wa Burundi wanaotaka kurudi nyumbani kwa hiari, na kusema kuwa wahusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Hata hivyo, UNHCR imesema imewasaidia wakimbizi wanaopenda kurudi nyumbani kwa hiari. Mpaka sasa wakimbizi karibu elfu 75 wamerudi Burundi tangu mwezi Septemba mwaka 2017.
Katika taarifa yake, shirika hilo linaeleza licha ya kwamba usalama umeimarishwa Burundi tangu kuzuka ghasia kufuatia uchaguzi mkuu mnamo 2015 " hali hairuhusu kushinikiza wakimbizi warudi Burundi".
Tanzania ndio nchi inayohifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka Burundi kuliko nchi nyingine yoyote ile katika ukanda wa Afrika Mashariki.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |