Mkutano wa kilele wa G7 wafungwa
Mkutano wa kilele wa mwaka 2019 wa kundi la nchi 7 (G7) umemalizika wiki hii mjini Biarritz nchini Ufaransa.
Taarifa iliyotolewa baada ya mkutano imesema masuala kadhaa yalijadiliwa ikiwemo masuala ya biashara, Iran, Ukraine na Libya, lakini haukupata matokeo halisi. Taarifa hiyo imesema kuwa kundi la nchi 7 litafanya juhudi kuendeleza biashara ya kimataifa yenye uwazi na haki na kulinda utulivu wa uchumi wa dunia.
Kabla ya kufungwa kwa mkutano huo, rais Donald Trump wa Marekani na rais Emmanuel Macron wa Ufaransa walikutana na waandishi wa habari kwa pamoja. Rais Macron amesema rais Hassan Rouhani wa Iran anataka kufanya mazungumzo na rais Trump, na Ufaransa itaendeleza juhudi za kuhimiza kufikiwa makubaliano kati ya Marekani na Iran.
Kwa upande wake, rais Trump alisema amepokea pendekezo la Ufaransa kuhusu kufanya mkutano na rais Hassan Rouhani wa Iran. Rais Trump alisema Marekani haitaki kuipindua serikali ya Iran, ila inachotaka ni Iran kutokuwa na silaha za nyuklia na makombora.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |