Saudi Arabia yaonesha mabaki ya droni kwenye miundombinu ya mafuta iliyoshambuliwa
Wizara ya ulinzi ya Saudi Arabia imetangaza wiki hii matokeo ya mwanzo ya uchunguzi wa tukio la mashambulizi dhidi ya miundombinu ya mafuta ya nchi hiyo, vilevile imeonesha mabaki ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyokusanywa kwenye maeneo yaliyoshambuliwa, na kuilaani Iran kupanga mashambulizi hayo.
Akiongea na wanahabari msemaji wa wizara ya ulinzi ya Saudi Arabia amesema dalili za mwendo wa makombora zimeonesha kuwa mashambulizi hayo yalitoka kaskazini mwa Saudi Arabia na sio Yemen kama ilivyotangazwa na kundi la Houthi, na baadhi ya makombora na ndege zisizo na rubani zilizotumiwa kwenye mashambulizi hayo zilitengenezwa na Iran. Ameongeza kuwa mashambulizi hayo yaliungwa mkono na Iran, lakini uchunguzi wa chanzo cha mashambulizi bado unaendelea, na matokeo ya mwisho ya uchunguzi bado hayajatolewa.
Kwa upande mwingine, waziri wa mambo ya nje wa Iran alipohojiwa na wanahabari alikanusha kwa mara nyingine tena juu ya Iran kushiriki kwenye mashambulizi hayo.
Kundi la Houthi la Yemen wiki hii limesema, miundombinu ya mafuta nchini Saudi Arabia iliyoshambuliwa bado ni shabaha ya mashambulizi ya kundi hilo.
Kundi hilo limebainisha kuwa, maeneo mawili waliyoshambulia hivi karibuni huenda yakashambuliwa tena wakati wowote, pia limezionya kampuni zilizoko kwenye maeneo hayo na wageni kuondoka. Vilevile limeitaka Saudi Arabia isitishe uvamizi na vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Yemen.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |