Serikali ya Kenya imeanza shughuli ya kutumia ndege kunyunyiza takriban lita 3,000 za kemikali kuangamiza mamilioni ya nzige waliovamia eneo la Kaskazini mwa Kenya huku wingu jingine kubwa la wadudu hao likionekana ambapo wamevamia Kaunti ya Meru na kuibua hofu miongoni mwa wakenya.
Akizungumza na vyombo vya habari, Msemaji wa serikali Kanali Cyrus Oguna amesema kwamba Rais Uhuru Kenyatta alikuwa amearifiwa kikamilifu kuhusu suala hilo na kwamba mikakati ya dharura imeanza kutekelezwa ili kukabiliana na suala hilo haraka iwezekanavyo.
Afisa huyo pia aliwahakikishia Wakenya kwamba serikali ilikuwa imedhibiti kikamilifu tatizo hilo la nzige huku akiwahimiza Wakenya kurejelea shughuli zao kama kawaida.
Haya yamejiri baada ya mamilioni ya nzige wa jangwani kutoka ama Ethiopia au Somalia kuvamia eneo la Kutulo, Kaunti ya Wajir baina ya Jumatano na Ijumaa wiki iliyopita katika hali iliyoibua taharuki eneo hilo.
Wingu la nzige hao alhamisi walivamia mashamba ya miraa katika kaunti ya Meru ,jambo lililozua wasiwasi miongoni mwa wakulima.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |