Mahakama moja ya Ufaransa imekataa ombi la mtuhumiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda Felicien Kabuga, kutaka aachiwe kwa dhamana wakati akisubiri uamuzi kuhusu mahali kesi yake itakaposikilizwa, baada ya kuukwepa mkono wa sheria kwa zaidi ya miaka 25.
Kabuga anatuhumiwa kufadhili mipango ya kufanya mauaji ya halaiki ya mwaka 1994, ambayo yaliangamiza maisha ya watu zaidi ya 800,000, wengi wao wakiwa kutoka jamii ya Watutsi, lakini pia Wahutu wenye msimamo wa kadri, katika muda wa siku 100.
Alifika mahakamani akisukumwa kwa kiti cha magurudumu, na kuiomba korti aachiwe kwa misingi ya afya mbovu na uzee, akisema ana umri wa miaka 87, ingawa rekodi rasmi zinasema umri wake ni miaka 84.
Mwendeshamashtaka wa Chombo cha Kimataifa kinachofuatilia kesi za uhalifu, Serge Brammertz amesema ikiwa atafurushwa nchini Ufaransa, Kabuga atafikishwa katika mahakama ya chombo hicho iliyopo mjini Arusha, Tanzania.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |