Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Ethiopia imesema watakaokiuka masharti yanayolenga kupunguza kusambaa kwa virusi vya corona ukiwemo uvaaji wa barakoa katika maeneo ya umma watafungwa jela hadi miaka miwili.
Masharti hayo mapya ya kudhibiti kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini humo ni pamoja na watu kuzuiwa kupeana mikono katika maamkizi, agizo la uvaaji wa barakoa katika maeneo ya umma, zuio la watu zaidi ya watatu kukaa katika meza moja kwenye mikahawa na maeneo mengine ya umma na uzingatiaji wa kukaa umbali wa futi sita baina ya watu wawili.
Lia Tadesse, Waziri wa Afya wa Ethiopia katika ujumbe wake wa Twitter alisema hatua ya kuondolewa hali ya hatari na kueleza bayana kuwa,Sasa hivi watu wanaishi kama kwamba hakuna tena Covid-19, umma hauchukui tahadhari. Hii inaweza kusababisha ongezeko la maambukizi na kuliweka taifa hatarini.
Nchi hiyo ya Pembe ya Afrika ilitangaza hali ya hatari kutokana na kasi ya kusambaa virusi vya corona mnamo mwezi Aprili mwaka huu, lakini ikaondolewa mwezi uliopita.
Takwimu za Wizara ya Afya ya Ethiopia zinaonyesha kuwa, hadi sasa taifa hilo limenakili kesi 91,118 za ugonjwa wa Covid-19, ambapo watu 1,384 walifariki dunia kwa corona.
Kadhalika wagonjwa wa corona waliopata afueni nchini humo ni zaidi ya 44,506.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |