Kenya yaunda kituo cha uongozi wa kukabiliana na dharura ya mafuriko
2023-11-29 08:42:42| CRI

Kenya imeunda kituo cha uongozi wa kukabiliana na dharura ya mafuriko, ili kurekodi na kuripoti taarifa yoyote kuhusu maafa ya mafuriko nchini kote, wakati idadi ya vifo vilivyosababishwa na mafuriko ikiongezeka hadi 120.

Katibu mkuu wa Wizara ya Usalama wa Ndani wa Kenya Bw. Raymond Omollo amesema timu ya kituo hicho inayojumuisha wizara 11 na mashirika yao husika itatoa tahadhari ya mapema na taarifa kuhusu usalama na mwitikio dhidi ya mafuriko kwa wadau na umma.

Pia amesema timu hiyo imepewa jukumu la kuhamasisha raslimali na kuunganisha uwezo katika ngazi zote za serikali na kushirikiana na mashirika husika ya serikali kuu na za kaunti ili kukabiliana na hali mbalimbali za dharura.