China ni nchi yenye makabila madogo madogo mengi. Ili kuwawezesha wanafunzi kutoka makabila hayo wazoee masomo na maisha ya vyuo vikuu, vyuo hivyo vimewaandalia madarasa maalumu. Bw. Shao Chunliang ambaye ana umri wa miaka 74 alikuwa profesa wa chuo cha mawasiliano ya simu cha Chuo Kikuu cha Ufundi Anuwai cha Dalian, na baada ya kustaafu, aliendelea na kazi ya kufundisha kwenye darasa la wanafunzi wa makabila madogo madogo watakaojiunga na chuo kikuu hicho. Bw. Shao Chunliang alisema, "Kama China inataka kupata maendeleo katika sekta mbalimbali, inapaswa kutilia mkazo elimu kwa wananchi wake, hasa kwa watu wa makabila madogo madogo."
Wanafunzi wa makabila madogo madogo kutoka kila pembe ya China wanakwenda Dalian mji ulioko kando ya bahari, wakiwa na kiu ya kupata elimu ya juu. Walipofika katika mji huo mwanzoni, waliona ugeni kwa kila kitu, lakini Bw. Shao huwakaribisha kwa upendo kama jamaa zake. Mwanafunzi kutoka kabila la Wamongolia Bai Yang alisema,
"Wakati nilipoanza masomo yangu hapa, nilishangaa sana kuona kuwa mwalimu Shao aliita jina langu mara tu nilipoingia darasani. Alinishika mkono na kuniuliza safari ilikuwaje kwa garimoshi. Baadaye nilitambua kuwa kabla ya kufika sisi wanafunzi wa makabila madogo madogo, mwalimu Shao alizisoma nyaraka zetu za utambulisho kwa makini, ndiyo maana anajua majina yetu hata kabla ya kukutana nasi."
Bw. Shao amewafundisha wanafunzi wa makabila madogo madogo kwa miaka 23. Katika siku za kawaida, kila alfajiri na mapema, Bw. Shao alitoka nyumbani kwake na kwenda kwenye mabweni ya wanafunzi wake, ili kuwaamsha na kufanya mazoezi ya kujenga mwili pamoja nao, adhuhuri, anakula chakula pamoja na wanafunzi hao na kufanya mazungumzo nao, na usiku anaondoka baada ya wanafunzi wake kulala. Wakati wa likizo, Bw. Shao huwasindikiza wanafunzi wake kurudi nyumbani mpaka kwenye kituo cha garimoshi. Wanafunzi wengi wanaishi mbali sana, na inawachukua zaidi ya siku tatu kufika nyumbani kwao kutoka Dalian kwa garimoshi, hivyo kila mara anawaandalia vyakula.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |