"Kwanza, hayo ni maporomoko ambayo yako katika nchi mbili, na yanawavutia watalii zaidi. Pili, maji yake ni mengi zaidi kuliko maji ya maporomoko maarufu ya Huangguoshu, tena namna yake ni ya kupendeza zaidi kwa kuwa na umbo la nusu mviringo."
Watalii wanaotembelea sehemu ya maporomoko ya Detian, licha ya kuweza kuona mandhari nzuri ya maporomoko ya maji, vilevile wanaweza kutembelea sehemu nyingine za karibu zenye vivutio, ukiwemo mto unaoitwa maji meusi ambao unaanzia katika wilaya ya Jingxi. Kama unakwenda huko katika majira ya joto, utaweza kuona baridi inayoletwa na maji ya mto. Mbali ya mto huu, kuna sehemu nyingine inayoitwa "Guilin ndogo", ambayo ina mandhari nzuri ya mashambani ikiwa ni pamoja na nyumba za wakulima, wakulima wanaofanya kazi mashambani na watoto wanaochunga ng'ombe malishoni.
Ni dhahiri kuwa umaalumu wa utalii kwenye sehemu ya maporomoko ya maji ni mila na utamaduni wa sehemu hii ya mpakani. Kwenye mto Guichun, ambao uko kwenye sehemu ya mtiririko ya chini, watalii wanaweza kuona wafanyabiashara wa Vietnam wanaouza sigara, manukato na chakula kwenye vyelezo vya mianzi. Ukitaka kuona pilikapilika za shughuli za biashara inayofanyika kwenye sehemu ya mpakani, unaweza kutembelea soko la Jiebei karibu na maporomoko ya maji ya Detian. Soko hilo liko kwenye mteremko, ambapo vimejengwa vibanda vingi rahisi, ambako kuna watu wanaofika kwenye soko hilo.
"Dada njooni mwangalie, unataka keki zilizotengenezwa kwa choroko? Kuna boksi iliyowekwa keki 6 na iliyowekwa keki 8."
Msichana mdogo wa Vietnam alikuwa akiwaita wateja kwa lugha ya Kichina. Mwaka huu ana umri wa miaka 12 na ameanza shule ya sekondari, baada ya shule kufunga anakuja kumsaidia baba yake, katika kibanda chao vimewekwa vitu vingi. Alimwambia mwandishi wetu wa habari, kati ya watu wengi wanaokuja kuuza bidhaa kwenye soko hilo, kuna wenyeji wa mkoa wa Guangxi, China, na Wavietnam wenye vitambulisho vya sehemu ya mpakani, katika soko hilo, watalii wanaweza kupata vitu vya Vietnam vinavyouzwa kwa bei nafuu.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |