Kuhifadhi na kuendeleza maliasili ya msitu pia ni kazi muhimu. Katika miaka 10 iliyopita, wilaya ya Mohe ilishiriki kwenye "mradi wa kuhifadhi misitu ya asili", kuzuia watu wesiingie mlimani kwa kipindi fulani ili kustawisha misitu ya mlimani, kupiga marufuku kukata miti, na kupunguza kwa kiasi kikubwa uzalishaji wa mbao za biashara, ili misitu ya asili iweze kupumzishwa na kustawi, wakati huohuo wilaya hiyo pia inapanda miti. Baada ya juhudi za miaka mingi, msitu ulioteketezwa umefufuka, na wilaya hiyo imejenga maeneo 9 ya hifadhi ya kimaumbile, ambapo sasa misitu imefunika asilimia 90 ya eneo la ardhi kutoka asilimia 61 ya zamani. Naibu mkuu wa wilaya ya Mohe Bw. Hou Zhenkun alisema,
"Katika miaka ya hivi karibuni, ili kuhifadhi maliasili ya misitu, wilaya ya Mohe inapunguza uzalishaji wa mbao mwaka hadi mwaka, wafanyakazi wa ziada wa misitu wamehamishiwa kufanya shughuli za utalii na utoaji huduma, hivi sasa mapato ya watu wanaoshughulikia mambo ya utalii wilayani Mohe ni makubwa zaidi."
Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu, sehemu ya Milima Daxing'anling ilitenga Yuan milioni 487 katika ujenzi wa hali ya viumbe, ilipunguza uzalishaji wa mbao zaidi ya mita milioni 2 za ujazo, wakati huohuo ilitumia raslimali za utamaduni wa huko na mazingira ya asili kuendeleza zaidi shughuli za utalii. Katika kijiji cha Beiji, ambacho ni sehemu yenye vivutio wilayani Mohe, familia zinazojihusisha na shughuli za utalii zimeongezeka kuwa 78 kutoka 20 za mwaka 2002. Mwaka huu, watalii waliotembelea wilaya ya Mohe wameongezeka kwa asilimia 70, na mapato ya utalii yameongezeka kwa asilimia 80.
Misitu ya Milima Daxing'anling ni kinga ya hali ya viumbe ya sehemu za kaskazini na kaskazini mashariki mwa China. Wilaya ya Mohe inafuatiliwa sana kutokana na kufufua maliasili ya misitu na kuboresha mazingira ya asili kwa miaka mingi. Mafunzo ya mwaka ule pamoja na uzoefu wa leo unaifanya wilaya ya Mohe iwe kituo cha kielelezo kwa sehemu zote nchini China. Mwazoni mwa mwezi Agosti mwaka huu, mkutano wa 2 wa baraza la ngazi ya juu kuhusu ujenzi wa ustaarabu wa ikolojia ulifanyika kwa mafanikio huko Mohe. Wataalam wa nchini na wa nchi za nje walijadili masuala kuhusu ustaarabu wa ikolojia na maendeleo endelevu ya uchumi na jamii, na uhusiano kati ya ustaarabu wa ikolojia na kuboresha maisha ya watu. Hivi sasa, wilaya ya Mohe imekuwa sehemu yenye umaalum ya ustaarabu wa ikolojia katika sehemu ya Milima Daxing'anling.
© China Radio International.CRI. All Rights Reserved. 16A Shijingshan Road, Beijing, China. 100040 |