Balozi Kairuki ashauri namna ya kutatua changamoto za biashara kwa njia ya mtandao
2020-01-17 09:14:27| CRI

Na Majaliwa Christopher

HUKU uwekezaji na biashara kati ya China na Tanzania ukiizidi kukua na kuimarika siku hadi siku, Balozi wa Tanzania jijini Beijing Mbelwa Kairuki ameshauri wafanyabiashara wa pande zote mbili kuwa makini hasa katika biashara kwa njia ya mtandao ili kuepuka changamoto za kuibiwa au kutapeliwa.

Ingawa, kwa mujibu wa Balozi Kairuki, katika mwaka uliopita, 2019, kulikuwa na taarifa chache juu ya kutapeliwa au kuibiwa hasa katika biashara kwa njia ya mtandao kati ya wafanyabiashara wa China na Tanzania, alisema ni muhimu kuchukua tahadhari ili mahusiano ya kibiashara kati nchi hiyo ya Asia ya Mashariki na Tanzania kuwa ya manufaa zaidi.

"Ubalozi unapenda kutoa angalizo kwa Watanzania wanaotaka kufanya biashara na makampuni ya Kichina wanayoyapata kwa njia ya mtandao kuchukua tahadhari ili kuepuka changamoto kama hizo," alisema Balozi Kairuki hivi karibuni katika taarifa yake maalum kwa wafanyabiashara wa Tanzania.

Balozi Mbelwa alitaja baadhi ya hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa katika tahadhari hiyo ikiwa ni pamoja na kupata jina kamili la kampuni unayotaka kufanya nayo biashara.

"Sisitiza kupewa jina la Kichina la kampuni husika kwani mfumo wa Msajjli wa Makampuni unatambua Majina ya Kichina tu. Vilevile ni vizuri ukapata majina kamili ya Kichina ya mhusika wa kampuni unayewasiliana naye. Pia muombe akupatie "weechat ID" yake," alishauri Bw. Mbelwa.

Aliongeza kuwa ni muhimu pia kufanya "due-dilligence" juu ya uwepo wa kampuni husika na kupata taarifa za uwezo wa kampuni hiyo kimtaji na rekodi ya biashara ya kampuni husika.

Alieleza kuwa kwa mfanyabishara yeyote anayetaka kuhitaji huduma hiyo ya"due-dilligence" anaweza kuwasiliana na Ubalozi wa Tanzania Nchini China au kwa kupitia kwa Ofisi ya Mwakilishi wa Uchumi na Biashara wa Ubalozi wa China nchini Tanzania, jijini Dar es Salaam.

"Baada ya kuthibitisha sifa na uwezo wa kampuni husika kufanya biashara inayokusudiwa; ni muhimu kuingia Mkataba wa Biashara," alisema Kairuki.

Mwakilishi huyo wa Serikali ya Tanzania nchini China pia aliongeza kuwa njia salama zaidi ya kufanya malipo ni "Letter of Credit" ili kuweza kuzuia malipo endapo muuzaji amekiuka makubaliano ya kimkataba.

"Kwa manunuzi makubwa yanayozidi USD 20,000 inashauriwa katika Mkataba kuweka kipengele cha "Pre-shipment Inspection" ili kujiridhisha kwamba bidhaa inayotumwa ndio sahihi uliyonunua," alifafanua Balozi Kairuki.