Rais Magufuli aielekeza kampuni ya CRJE ya China kumaliza kazi kwa wakati
2020-01-17 09:13:52| CRI

Na Majaliwa Christopher

RAIS wa Tanzania Dkt. John Magufuli Jumamosi, Januari 11, 2020 aliweka jiwe la msingi la shule ya Sekondari ya Mwanakwerekwe iliyopo Zanzibar inayojengwa na Kampuni ya China Railway Jianchang Engineering Company Limited (CRJE).

Uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa shule hiyo imefanywa siku mbili baada ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein nae kushiriki hafla ya ufunguzi wa shule ya sekondari ya Mwembeshauri iliyojengwa na Kampuni ya Group Six International Limited kutoka China.

Ujenzi wa shule hiyo iliyofunguliwa na Dkt. Shein ulitekelezwa kwa mashirikiano kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wahisani Opec Fund for International Developement (OFID), kupitia mradi wa Zanzibar Third Education Project (ZATEP) na iligharimu jumla ya Shilingi Bilioni 3.5 za Tanzania.

Akizungumza katika shughuli hiyo mwishoni mwa wiki, Rais Magufuli aliielekeza mkandarasi anayejenga majengo hayo --kampuni ya CRJE kutoka China ambayo ilipaswa kukamilisha ujenzi huo tangu Agosti 2019 kuhakikisha inakamilisha kazi ifikapo Machi 2020 kama ilivyoahidi.

"Naomba kampuni ya CRJE ya China kukamilisha hii kazi kama ilivyoahidiwa ili kutoa fursa kwa watoto wetu wa Tanzania kusoma bila changamoto yoyote ya kimiundombinu," alielekeza Dkt. Magufuli.

Shule ya Sekondari Mwanakwerekwe inayojengwa na CRJE ya China ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 960 na inajengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 2 na Milioni 628.

Mradi huo ni moja kati ya shule 24 zinazojengwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ufadhili wa Benki ya Dunia chini ya mradi wa kuinua kiwango cha elimu Zanzibar.

Akizungumza baada ya kuweka jiwe la msingi na kukagua majengo ya Shule ya Sekondari Mwanakwerekwe, Rais Magufuli alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Shein kwa juhudi kubwa za kuiletea maendeleo Zanzibar ikiwemo utekelezaji wa mradi huo na ameeleza kuridhishwa kwake na ubora wa majengo yanayojengwa.

Hata hivyo, Rais Magufuli alielezea kutoridhishwa na matokeo ya shule za Zanzibar kushika nafasi za chini katika ufaulu wa mitihani ya Kitaifa na hivyo kutoa wito kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar Bi. Riziki Pembe Juma pamoja na wataalamu wake wa Wizara kufanyia kazi changamoto hiyo ili shule za Zanzibar zifanye vizuri katika mitihani hiyo.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli aliwapongeza viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha nchi inatulia na amewataka Wazanzibari wote kudumisha amani kwani bila amani nchi haiwezi kufanya maendeleo ikiwemo utalii ambao unachangia asilimia 80 ya fedha za kigeni za Zanzibar na asilimia 27 za Pato la Taifa.