China yatangaza fursa ya vijana wa Tanzania kupata uzoefu wa maandiko ya biashara ili kujiajiri
2020-01-17 09:13:17| CRI

Na Theopista Nsanzugwanko, DAR ES SALAAM

CHINA imetangaza fursa kwa vijana wa Tanzania kwenda nchini China kuongeza uzoefu maandiko ya kibiashara ili waweze kujiajiri kuliko kutegemea kuajiriwa na Serikali.

Balozi wa China nchini Tanzania Bibi Wang Ke wakati akifungua kituo cha Mawazo ya Kibiashara (Business Incubator) kilichoanzishwa na Chuo Cha Uhasibu Mkoani Arusha (IAA).

Bibi Wang Ke anasema milango iko wazi kwa vijana kwenda nchini China kupata uzoefu katika masuala ya biashara kwani vijana wengi wa nchini China wameendelea kwa kujiajiri na sio kuajiriwa.

Anawataka vijana wa kitanzania kuanzisha mawazo ya kibiashara ya viwanda vidogo vidogo vyenye mtaji kidogo kwani hiyo ndio njia pekee ya kujiajiri.

Balozi huyo anasema katika nchi ya China yenye watu zaidi ya bilioni moja ina vijana wengi lakini asilimia kubwa wamejiajili kwa kuwa na mawazo ya kibiashara yenye mtaji mdogo wenye kuanzisha viwanda vidogo vidogo.

Anasema viwand ahivyo vimesaidia kuwainua kiuchumi hivyo ni fursa kwa vijana wa kitanzania kwenda China kupata uzoefu na hatimaye kurejea nchini na kujiajiri kuliko kutegemea kuajiriwa.

Naye Balozi wa Tanzania Nchini China, Bw. Mberwa Kairuki anasema nchini China kuna fursa nyingi na kutaka vijana wa Tanzania kutumia mwanya uliotolewa na serikali ya China kwenda nchini humo kupata uzoefu wa mawazo ya kibiashara ili waweze kujiajiri.

Balozi Kairuki anasema kuwa serikali itakuwa bega kwa bega na vijana katika kuwasaidia kwenye mawazo ya kibiashara kwa lengo la kuhakikisha vijana wanajiajiri na sio kutegemea ajira serikalini.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo anawashukuru mabalozi wote kwa kuhamashisha vijana kujiajiri na kutoa fursa kwa vijana kwenda China kupata uzoefu katika masuala ya kibiashara yenye lengo la kujikwamua kiuchumi.

Gambo anasema vijana wana ari ya kujifunza mawazo ya kibiashara na kujifunza zaidi teknolojia ya kisasa ili waweze kuwa mabalozi wazuri kwa wenzio ilsa walimu nao wanapaswa kusaidiwa pia katika hilo.

Anasema walimu nao wanapaswa kupata ujuzi zaidi katika mawazo ya kibiashara na kujua teknolojia za kisasa maana dunia inakwenda kasi sana kwa masuala ya teknolojia hivyo wanawajibu wa kwenda nje ya nchi kujifunza zaidi.

Mkuu wa Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA) Profesa Eliamani Sedoyeka anasema mbali ya kuwafundisha masomo mengine chuo kimekuwa kikisisitiza elimu ya mawazo ya kibiashara yenye lengo la kutaka vijana kujiajiri

Anaishukuru China kwa kutoa fursa kwa vijana kwenda katika nchi hiyo kupata uzoefu zaidi wa masuala ya biashara ili waweze kuwa wakombozi wa wengine hapa nchini.