Ujasiri wa uongozi wa China kwenye vita dhidi ya janga la COVID-19
2020-04-01 08:51:42| CRI

Ujasiri wa uongozi wa China kwenye vita dhidi ya janga la COVID-19

Na Eric Biegon – NAIROBI

Uwezo wa uongozi wowote popote huonekana katika nyakati za migogoro. Ama kwa hakika, ni katika nyakati za dhiki ndipo serikali zinaimarishwa au kusambaratishwa. Hali kama hii pia inaonekana katika taasisi mbali mbali, ziwe za kisiasa, kiuchumi au kijamii.

Mwaka 2020 inaonekana kuwa mwaka uliotoa changamoto kubwa zaidi kwa taifa la China kwa kipindi cha muda mrefu.

Mkurupuko wa virusi vya corona uligubika mkoa mmoja wa China huku ukitishia kusambaza madhara yake katika sehemu nyingine ya nchi hiyo. Kwa sababu ya tishio hili, hakukuwa na budi ila kuchukuliwa kwa hatua madhubuti, na kwa kasi, ikiwa janga hilo lingedhibitiwa na kuzuiwa kutoenea kwa haraka na kuangamiza mamilioni ya watu.

Si siri kwamba janga hili ni kumbwa mno, lakini chama cha kikomunisti cha China (CPC) chini ya uongozi wa Rais Xi Jinping imeonyesha uwezo sawia kudhibiti hali. Waangalizi wengi wanahoji kuwa uongozi wa Rais Xi ulikuwa muhimu kwa nchi hiyo kufanikisha mapambano hayo.

Kwa kila hali, hii ilikuwa ni vita. Ilikuwa mapambano ya kuokoa maisha ya watu wapatao 1,400,000,000. Chama tawala ililazimika kufanya kila liwezalo kufanikisha vita hivyo. Na kama ilivyoonekana katika majanga ya awali, CPC ilitumia nguvu zake na rasilimali zilizoko mikononi mwake kwa shughuli hiyo.

Matokeo yake yamekuwa ya kuridhisha, kwani toka Machi 18 hakuna visa vipya vya mkurupuko huo vinavyoripotiwa nchini China. Shirika la afya duniani WHO limetoa pongezi mafanikio hayo na kusema, yanawapa walimwengu matumaini.

Sio siri kwamba mwanzoni, hatua zilizochukuliwa na China kupambana na chamuko hilo zilikosolewa pakubwa. Hata hivyo, kutokana na hali ya sasa hasa katika maeneo mengi ya Ulaya, Amerika, na sehemu nyingine za Asia, dunia yote imesadiki kimo cha changamoto iliyoko na kukubaliana na juhudi zilizochukuliwa na China kuzuia kusambaa kwa COVID-19.

Mwezi Februari, vinara wa chama tawala cha CPC katika mkoa wa Hubei walisimamishwa kazi kwa kile kilichotajwa kuwa utepetevu  katika hatua za awali za kupambana na chamuko hilo.

Baada ya kuondolewa kwao, serikali ilizindua mikakati muafaka ya kuhakikisha virusi hivyo vimekwamishwa. Chama tawala cha CPC, chini ya uongozi wa Rais Xi, iliamuru matumizi ya rasilimali za nchi kukabiliana na janga hilo.

Kwa haraka, kwa amri ya Rais Xi Jinping jeshi la China lilituma kikosi cha wanajeshi matabibu kwenye Wuhan, ambao ni mji mkuu wa mkoa Hubei na pia ni kitovu cha mkurupuko huo. Baadhi yao waliwahi kwenda Afrika kuchangia mapambano dhidi ya Ebola.

Januari 23, mamlaka ziliamrishwa kuhakikisha udhibiti kamili wa hali na kudumisha amri ya watu kutotoka nje kiholela, na serikali ya China iliyo na makao yake jijini Beijing ilitangaza kusimamishwa kwa usafiri wote wa umma zikiwemo usafiri wa ndege na treni. Katika hatua isiyo ya kawaida, wakaazi wa mji wa Wuhan waliwekwa chini ya karantini.

Baada ya kufungwa kwa maeneo yote, mamlaka mkoani Hubei ilianza shughuli za kusafisha miji ili kuua viini vya maradhi, na kila mkzai kupimwa virusi vya corona bila malipo, huku hospitali maalum zikijengwa, na kliniki maalum zikiasisiwa ili kushughulikia wale walioambukizwa mbali na familia zao.

Ndani ya siku 10, hospitali yenye vitanda 1,000 ilijengwa kwa ajili ya kuwapokea wagonjwa wenye hali mbaya zaidi, na hospitali nyingine ya namna hii yenye vitanda 1,500 ilijengwa ndani ya siku 15. Na majumba ya michezo yalitumiwa kuwa kliniki maalumu ya muda ya kuwapokea wagonjwa ambao hali yao si mbaya.

Serikali ilionekana kupuuza kanuni za kawaida za kukabiliana na mikurupuko. Baadhi ya wakosoaji walionya kwamba mbinu hii haikuwa nzuri na ingeweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi.

Lakini hatua hizi madhubuti kwa mujibu wa Rais Xi Jinping zilihitaji "ujasiri mkubwa wa kisiasa." Yeye anasisitiza kwamba hatua zisizo za kawaida zilistahili kuchukuliwa kwani "vinginevyo, tungejipata katika matatizo zaidi."

Kiongozi huyo wa China aliongoza mikutano kadhaa zikiwa ni pamoja na vikao mbalimbali na kamati ya Politburo, ambacho ni chombo cha juu cha kufanya uamuzi wa chama cha kikomunisti cha China. Na hapa kulikuwa na ajenda moja tu kwenye meza, jinsi ya kupambana na COVID-19.

Aidha, Xi aliwahamasisha wanachama 90,000,000 wa chama tawala kutoa mchango wa kifedha kuelekea katika kukabiliana na janga hilo, nae na viongozi wengine wa China walitangulia kutoa mchango.

Kwa kutii wito huu, ndani ya wiki moja, zaidi ya wanachama 42,000,000 wa chama cha kikomunisti cha China walikuwa wametoa mchango wa hiari wa Yuan 4,730,000,000, sawa na dola za kimarekani milioni 650.

Kampeni hiyo ya mchango imekuwa inaendelea, na inatarajiwa kuendelea hadi ushindi utakapotangazwa dhidi ya ugonjwa huo.

Chama hicho pia kiliamuru kupelekwa kwa madaktari 42,000 kutoka mikoa yote ya nchi kuelekea Hubei. Wataalam kutoka nyanja nyingine walielekea mji wa Wuhan kusaidia katika njia nyingine tofauti. Vifaa vya matibabu na mahitaji yote ya maisha kama vile chakula vinasafirishwa hadi Hubei kutoka sehemu mbalimbali ya China, na seriklai ya mitaa iliwashirikisha vijana waliojitolea kupeleka mahitaji hayo hadi familia moja baada ya nyingine. Kwa hiyo wakazi wa Wuhan waliowekwa karantini walipata mahitaji ya kila siku bila kutoka nje.

Hii ndiyo sababu hospitali zilijengwa haraka. Katika muda wa rekodi, kumbi za michezo zilibadilishwa kuwa vituo vya afya.  Ndio, kwa muda mfupi zaidi, bidhaa vya kimatimabu na vingine vilivyohitajika kusaidia walioambukizwa vilifikishwa eneo hilo. Ndio, wakazi walikuwa hiari kufuata amri ya serikali ya kutoka nje.

Hatua hizo zilizochukuliwa na uongozi wa China zilipokea sifa kutoka kwa shirika la afya duniani, WHO.

Akizungumza na jarida la New York Times, Dkt. Bruce Aylward ambaye alikuwa kiongozi wa kikosi cha WHO kilichozuru China mwanzoni, alibainisha kwamba mkurupuko uliokuwa ukisambaa kwa kasi ulidhibitiwa kwa haraka kinyume na matarajio ya wengi. Alisema mamia ya maelfu ya watu nchini China waliepuka maambukizi ya COVID-19 kwa sababu ya hatua kali zilizochukuliwa na serikali.

Akichanganua muda aliokuwa nchini China, Dkt. Aylward alihitimisha kwa kusema "China ni kielelezo katika kuhakikishia watu wake uhai."

Alisema hatua za China za kupambana na mkurupuko huo ni za kuigwa.

Kwa hatua zinazohitaji kupongezwa, serikali ya kikomunisti ya China iliondoa mzigo kutoka kwa raia wake wakati ilipotangaza wazi kwamba yeyote atakayethibitishwa kuwa na maradhi hayo, hapaswi kuwa na wasiwasi kuhusu gharama ya tiba kwani ni bure.

Xi na chama tawala waliondoa kila shaka na kudumisha kwamba maisha ya watu yalipewa kipaumbele zaidi na kwamba hii ilitangulia kila kitu kingine.

Katika kampeni kali sana, na isiyo na kifani, ambapo watu walichunguzwa na kupimwa na miji kusafishwa, China ilipunguza visa vya COVID-19 katika mipaka yake kutoka 15000 katikati ya Februari hadi sifuri katikati tarehe 18 mwezi Machi.

Na kwa kuwa mkurupuko huo kwa sasa umedhibitiwa, China sasa inaelekeza macho yake kwa ujenzi wa uchumi wake, na kusaidia nchi nyingine duniani ambazo maambukizi ya ugonjwa huo yanaendelea.

Mataifa ulimwenguni yanaweza kuiga mikakati ya lazima yaliyotekelezwa na uongozi wa China ili kuzuia kuenea kwa COVID-19.