China yahimiza ushirikiano wa kimataifa kukabiliana na mgogoro wa kiafya na kiuchumi
2020-05-30 17:39:13| CRI

China yahimiza ushirikiano wa kimataifa kukabiliana na mgogoro wa kiafya na kiuchumi

Janga la virusi vya Corona, kwa sasa, limeibuka kuwa changamoto kubwa zaidi ambalo wanadamu wamekumbana nalo tangu vita vikuu vya dunia. Ugonjwa huo wa kuambikiza umesambaa hadi karibu kila kona ya dunia. Hadi sasa, nchi 213 na maeneo kote duniani yameathirika.

Popote ambapo mlipuko wa ugonjwa wa covid-19 umeripotiwa, maisha kamwe hayabaki sawa. Janga hili limeacha uharibifu mkubwa katika mapito yake. Takriban watu 360,000 wamekufa kutokana na ugonjwa huo huku zaidi ya watu 5,900,000 hadi sasa wakithibitishwa kuambukizwa virusi hivyo.

Bila chanjo, mataifa yameachwa bila jingine ila tu kupigana kuzuia kuenea kwake.

Hata hivyo, si suala la afya ya umma tu lililojawa mgogoro kwani janga hili limezorotesha uchumi wa dunia. Mamilioni ya watu wamepoteza kazi na chanzo cha mapato, na la kusikitisha zaidi, ni kwamba bado haijulikani ni wakati gani hali ya kawaida itarejea.

Huku hali ikiendelea kuzorota, miito kadhaa imetolewa wa kuwepo utekelezaji wa mpango wa pamoja wa kimataifa ili kukabiliana na changamoto zilizopo. Na baada ya kunakili kisa cha kwanza cha mkurupuko huo, China inaongoza kampeni hii.

Akihutubia mkutano wa waandishi wa habari baada ya hitimisho la mkutano wa kila mwaka la bunge la umma la China NPC, na baraza kuu la mashauriano ya kisiasa nchini humo (CPPCC), Waziri Mkuu wa nchi hiyo Li Keqiang alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika kupambana na ugonjwa wa covid-19 ili kuhakikisha ushindi dhidi ya janga linaloghubika dunia kwa sasa.

Kwa mujibu wa Li "jumuiya ya kimataifa sasa inakabiliwa na changamoto mbili, moja ikiwa ni kuenea kwa virusi hivyo na nyingine ikiwa ni juhudi za kurejesha uchumi na utaratibu wa kijamii."

Waziri Mkuu huyo, ambaye aliwasilisha ripoti ya kazi ya serikali ambayo baadaye ilipitishwa na wabunge wakati wa kikao hicho, anasema hali ya sasa inaweza tu kukabiliwa vyema kupitia mshikamano wa jamii ya kimataifa ikizingatiwa kuwa chamuko la corona na machafuko ya kiuchumi yanayoshuhudiwa yamekumba ulimwengu mzima.

"Haiwezekani kwa nchi yoyote kuafikia maendeleo yoyote ikiwa milango yake yamefungwa. China itaendelea kudumisha sera yake ya ufunguzi na wala haitatikiswa katika kutimiza ahadi hii." Alisema.

Huku akikiri kuwa masuala yote mawili yana ulinganifu, Waziri Mkuu Li Keqiang alisema kuwa ushirikiano wa pamoja ndio kipengele muhimu utakaohakikisha mataifa yameandikisha ushindi dhidi ya vitisho hivyo.

Alitumia fursa hiyo kutangaza kuwa China iko tayari kwa ushirikiano wa kimataifa hasa juu ya "utafiti na maendeleo ya chanjo, upatikanaji wa dawa na upimaji wa tiba ya kupambana na covid-19, na kwamba China iko tayari kushiriki matokeo mahsusi ya juhudi hizo."

Ahadi hii ya Li ilitolewa baada ya Rais wa China Xi Jinping kusisitiza umuhimu wa jitihada za pamoja katika kupambana na chamuko la Corona, huku akionya kuwa ugonjwa huo hauna mipaka.

'Jibu la pamoja tu kutoka jumuiya ya kimataifa linaweza kushinda janga hili, ' Kiongozi huyo wa China alisema.

Rais Xi, ambaye alishiriki majadiliano na wabunge pamoja na washauri wa kisiasa wakati wa mkutano wa bunge, alisema China iko tayari kuratibu jitihada katika suala hili pamoja na kutoa msaada wa vifaa kadri ya uwezo wake.

Na huku kukiwa na shutuma kwamba China ilificha habari kuhusu kiwango cha mlipuko huo wa corona, kiongozi huyo alishikilia msimamo kuwa nchi yake imekuwa ikitoa taarifa kwa njia ya "uwazi, na kwa uwajibikaji kuhusu kukurupuka kwake, sifa zake, utambuzi pamoja na mpangilio wa matibabu."

Rais huyo anashikilia kuwa taifa hilo lenye uchumi mkubwa zaidi barani Asia lina nia ya ushirikiano katika mapambano ya kimataifa dhidi ya ugonjwa huo huku akifichua kuwa China imetoa maarifa, msaada wa vifaa, na wataalamu kwa takriban mataifa 100 na mashirika ya kimataifa tangu kuzuka kwa maradhi hayo.

Xi alitoa wito zaidi wa jitihada za kudumu za kufanya mtandao wa kiuchumi kuwa wazi zaidi, pamoja na kuhakikisha usawa ili faida zake ziwafikie wote, na kujenga jamii yenye mafanikio ya pamoja.

Baada ya kudhibiti na kurejesha hali ya kawaida nchini China, viongozi hao wawili wanasisitiza kwamba Beijing itatoa mafunzo muhimu kuhusu ugonjwa wa covid-19 na jinsi ya kukabiliana nayo.

Hisia hizi zinalingana na maoni mbali mbali yaliyotolewa na wataalamu kote duniani wanaoshikilia mtazamo kwamba, ili kukabiliana na mgogoro wa sasa, kuna haja ya moyo wa ushirikiano na uaminifu.

Kwa hili, China haitoi pendekezo tu. Itakumbukwa kwamba serikali ya China iliongoza jitihada za kimataifa za kuzalisha na kusambaza vifaa vya matibabu, hasa, vifaa vya kupima hali mwilini na vifaa vya kusaidia kupumua. Juhudi za mfanyabiashara maarufu Jack Ma pia zimegonga vichwa vya habari kote ulimwenguni.

Wito huu wa China unalingana na maombi ya wengi ambao wanahoji kuwa nchi tajiri vinafaa kuwa tayari kutuma vifaa vinavyohitajika sana kwa nchi maskini zinazotatizwa na ugonjwa huo.

Aidha, kumekuwa na miito kwa Mataifa kuzingatia kuwaleta pamoja matabibu. Chini ya pendekezo hili, nchi ambazo hazijaathirika pakubwa kwa sasa zinaweza kuwapeleka wafanyakazi wa afya katika maeneo yanayoathirika zaidi ulimwenguni, ili kuwasaidia katika wakati huu pamoja na kutoa uzoefu wa thamani.

Wale wanaounga mkono hoja hii pia wanasisitiza kuwa ushirikiano wa kimataifa ni muhimu sana kwa upande wa kiuchumi. Huku ikifahamika fika kuwa uchumi wa dunia ni mtandao, hoja imetolewa kwamba iwapo kila serikali itafanya kazi kwa kupuuza wengine, matokeo yatakuwa vurugu na kuongezeka kwa mgogoro.

Inaonekana, mgogoro wa sasa unatoa fursa mahsusi kwa mataifa kutambua hatari unaotokana na utengano. Inawezekana sana kwamba kutokuwa na umoja kwa wakati huu unaweza kuongeza mgogoro, ilihali mshikamano, inaweza kuwa njia pekee ya ushindi dhidi ya covid-19.

China yahimiza ushirikiano wa kimataifa kukabiliana na mgogoro wa kiafya na kiuchumi