Msichana Atoroka Ndoa ya Kulazimishwa
2020-09-04 19:57:05| CRI

Msichana Atoroka Ndoa ya Kulazimishwa

Msichana mwenye umri wa miaka 17 anayeishi mkoani Guangdong amefanikiwa kukimbia ndoa ya kulazimishwa aliyopangiwa na wazazi wake, baada ya kutafuta msaada wa kisheria.

Msichana huyu anayejulikana kama Bibi Zhang aliandika kuhusu uzoefu wake huo wa kusikitisha kwenye makala iliyochapishwa kwenye gazeti la Hongxing News wiki hii. Amesema jinamizi hilo lilianza mwezi Februari, baada ya wazazi wake kumwambia kuwa wameanza kumtafutia mume. Licha ya yeye mwenyewe kupinga, wazazi wake walimkutanisha na kijana mwenye umri wa miaka 22 anayeishi katika kijiji kilicho karibu na nyumba yao. Baada ya kukutana na kijana huyu mara sita, msichana Zhang aliambiwa na wazazi wake kuwa tayari wamepokea zawadi za uchumba kutoka kwa familia ya kijana huyo.

Kinyume na nia yake, wazazi wa msichana huyo walimpangia harusi ifanyike Juni 2. Kabla ya sherehe za harusi kufanyika, Bibi Zhang alijaribu kubadili mawazo ya wazazi wake kwa kuwaambia kwamba hajatimiza umri wa kisheria wa kufunga ndoa kwa mujibu wa sheria za China. Hata hivyo wazazi wake bado walishikilia msimamo wao.

Ikiwa ni juhudi yake ya mwisho, msichana huyo alitafuta kisingizio cha kwenda kufanya manunuzi na kuondoka nyumbani siku moja kabla ya harusi kufanyika. Lakini badala ya kwenda kufanya manunuzi kama alivyowaambia wazazi wake, Bibi Zhang alikwenda katika ofisi ya Chama cha Wanawake katika mji wake kutafuta msaada. Muda mfupi baadaye, maofisa wa polisi waliingilia kati jambo hili na kuwasiliana na wazazi wake, ambao hatimaye wakaamua kufuta ndoa hiyo.

Uzoefu huo wa Bibi Zhang umezusha mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii nchini China, ambapo watumiaji wa mitandao hiyo wamesema jambo hilo limefichua masuala kadhaa makubwa yanayowakabili wanawake wa China, haswa wale wanaishi katika maeneo ya vijijini, ambako wasichana huhimizwa kuolewa baada ya kuzidi miaka ya 20.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa ya China, wanawake na wanaume wanaruhusiwa kufunga ndoa baada ya kufikia umri wa miaka 20 na 22 mtawalia. Baadhi ya wabunge wamependekeza kupunguza kikomo cha umri wa kufunga ndoa hadi kufikia miaka 18 kwa jinsia zote mbili. Lakini pendekezo hilo halikupitishwa kutokana na upinzani kutoka kwa vijana, ambao wamesema mabadiliko haya hayataathiri maamuzi yao ya kufunga ndoa na kupata mtoto, kabla ya kupata uhakikisho wa kifedha na utayari wa kiakili.