Kenya na China zasisitiza haja ya ushirikiano wa kimataifa
2020-09-28 10:04:05| CRI

Na Eric Biegon - NAIROBI

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na mwenzake wa China Xi Jinping wameelezea wasiwasi wao kuhusu kudhoofika kwa ushirikiano wa Kimataifa, hatua ambayo wamesema utaacha ulimwengu katika hali hafifu hasa kutokana kwa shinikizo zinazohatarisha utulivu wake.

Wakitoa hoja zao kuhusu umuhimu wa mshikamano thabiti wa kimataifa, viongozi hao wa nchi waliendeleza wito wa uwazi zaidi na umoja kama njia mahsusi ya kushinda changamoto zinazowakabili wanadamu kama vile ugaidi, magonjwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Walisema hili ni swala linalohitaji kupewa kipaumbele hasa ikizingatiwa kuwa nchi zinazidi kuunganishwa na kutegemeana, na kwamba hatima zao zimeunganishwa.

Jumbe hizi zilitolewa na viongozi hao kwa hafla tofauti mapema wiki hii katika taarifa za video zilizorekodiwa wakati wa mkutano mkuu wa kikao cha 75 cha mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Rais Kenyatta alisema ulimwengu unaweza kushinda changamoto kubwa zinazoikabili hivi sasa kama tatizo la afya la Covid-19 na mabadiliko ya hali ya hewa kupitia juhudi za pamoja za kimataifa.

"Ikiwa tutaendeleza muungano na umoja wenye nia njema...na iwapo tutakita mizizi katika mfumo wa kimataifa unaotawala na kutenda bila ubinafsi, basi tutaweza kutatua changamoto zetu na kupata amani na ustawi wa kudumu kwa wote," Alisema.

Kulingana na Rais Kenyatta, hatua madhubuti ya pande nyingi katika mfumo wa kimataifa ni ufunguo utakaofanikisha ushindi dhidi ya changamoto za ulimwengu mzima ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa amani na ustawi wa kudumu.

Hisia hizi zinalingana na zile za Rais Xi Jinping ambaye alihimiza mataifa kushikilia msimamo wa pande nyingi, akisisitiza hitaji la ulimwengu kukubali na kutekeleza dhana ya utawala wa ulimwengu kulingana na kanuni ya mashauriano, mchango wa pamoja, na faida za pamoja.

"Hatma ya ulimwengu inapaswa kuwa mikononi mwa wote; kitabu cha sheria cha kimataifa kilichoandikwa na wote; mambo ya kimataifa kujadiliwa na wote; na mgao wa maendeleo unaowashirikisha wote, badala ya kuruhusu nchi moja kutawala zaidi." Kiongozi huyo wa China alisema

Marais hao wawili walitaja malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa kama mfano wa hatua za kimataifa ambazo zinaonyesha matarajio ya ulimwengu ya kumaliza umaskini na kuhakikisha ustawi kwa wote.

Wakizungumzia usumbufu uliosababishwa na janga la COVID-19, marais hao pia walitaka kuimarishwa kwa utayari wa ulimwengu kukabiliana na kuongezeka kwa mizozo ya kiafya, huku wakibainisha kuwa janga hilo linapaswa kutoa msukumo mpya kwa juhudi za pamoja za kuongeza ushirikiano wa kimataifa.

"Maambukizi yanaendelea kuongezeka na vifo vinaendelea kuongezeka. Mgogoro wa kiafya ambao ni wa kihistoria katika karne hii umedhihirisha ukweli kwamba jamii ya wanadamu ni jamii yenye maisha ya baadaye, na kwa kuungana mikono tu ndipo nchi zote zinaweza kujiondoa katika janga hili." Rais wa China alisema

Kenyatta alionekana kuunga mkono maoni haya. Katika ujumbe wake, rais wa Kenya alisema kuwa "janga la Covid-19 na changamoto zingine za wakati huu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa usawa wa kijamii na kiuchumi, shida ya uhalali na utawala pamoja na udhaifu wa ulimwengu wetu wa dijitali umeonyesha upya umuhimu wa hatua za pande nyingi kuja pamoja."

Lakini hata baada ya kushughulikia awamu ya hali mbaya iliyosababishwa na Covid-19, walisema ulimwengu lazima ubaki pamoja kwa nia ya kufufua hali yake na misingi yake.

Wakati huo huo, Xi na Kenyatta walisisitiza hitaji la mataifa kuthibitisha kujitolea na kulinda uwepo wa Umoja wa Mataifa wakisema UN ni shirika la kimataifa lenye uwakilishi na lenye mamlaka zaidi.

Rais Xi haswa alibaini kuwa UN ni jukwaa muhimu zaidi wa kimataifa kuhimiza amani, na kushughulikia maswala ya kikanda na ya ulimwengu.

"Ili kudumisha umoja wa mataifa, ulimwengu unapaswa kulinda mamlaka ya UN. Kwa miaka 75 iliyopita, jukumu zuri linatotekelezwa na UN limekuwa dhahiri kwa wote, kutoa msukumo mkubwa na pamoja urithi muhimu kwa jamii ya wanadamu." Alisema

Kupitia shirika hilo, Xi alisema kuwa nchi zote ulimwenguni zimeimarisha uhusiano wa karibu na ushirikiano wa kina huku akisadiki kuwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii yamepiga hatua kubwa kusonga mbele.

"Kutatua matatizo ya ulimwengu kunahitaji suluhisho la ulimwengu. Na hakuna mahali bora zaidi kuliko Umoja wa Mataifa kwa jamii ya kimataifa kutafuta suluhisho hizo." Kiongozi huyo wa China alisema

Alisema mashirika maalum ya UN kama Shirika la Afya Ulimwenguni WHO yana jukumu lisiloweza kubadilishwa na kwa hivyo mataifa yanapaswa kuhilinda dhidi ya wale walio na nia ya kuidhoofisha.