China kuongoza mapambano ya kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi
2020-11-09 08:40:41| cri

Na Eric Biegon - NAIROBI

Muda mrefu baada ya vituo vya uchaguzi nchini Marekani kufungwa, ulimwengu bado haujui ni nani atakayekuwa rais wa taifa hilo. Lakini wakati ambapo dunia nzima lilikuwa likikodolea macho uchaguzi wa Marekani, tukio lingine lenye umuhimu mkubwa lilitokea.

Taifa hilo lenye uchumi mkubwa duniani liliaga rasmi mkataba wa Paris kuhusu hali ya tabia nchi. Baada kutuma ombi kwa Umoja wa Mataifa kujiondoa mnamo Novemba 4, 2019, muda wa ilani ya kutalikiana uliwadia rasmi siku moja baada ya uchaguzi, na Marekani sasa iko nje ya jukwaa la kimataifa la mabadiliko ya tabia nchi.

Mkataba huo wa mwaka 2015, ni makubaliano ya pamoja kati ya nchi 197 ambazo zinalenga kuzuia halijoto ya dunia kupanda zaidi ya viwango vilivyoamuliwa na wanasayansi na ambavyo vinatajwa kuwa hatari. Madhara yake mabaya yanayoonekana kupitia matukio ya hali ya hewa yaliyokithiri, kama vile vimbunga vya kuchoma, joto kali na ukame, mioto inayoenea mwituni na viwango vinavyoongezeka vya bahari.

Huku ikisadikika kuwa Marekani sasa haimo kwenye mkataba huo, wanadiplomasia wa hali ya hewa wameachwa wakijikuna vichwa hasa kuhusu mustakabali wa mipango ya kimataifa ya kukabiliana na changamoto hii. Mengi yamo hatarini na mazungumzo yamekithiri kuhusu ni nani aliye na uwezo wa kujaza nafasi hiyo iliyoachwa wazi.

Kutokana na kuongezeka kwa ushawishi wake wa kisiasa na kiuchumi duniani, China inaonekana kama taifa linalofaa zaidi kuongoza ajenda hiyo pamoja na masuala mengine ya kimataifa.

Na inatarajiwa kwamba taifa hilo la Asia Mashariki litachukua hatamu za uongozi na kuelekeza mataifa mengine katika mchakato wa kuzingatia hatua za uamuzi juu ya mabadiliko ya hali ya hewa. Lakini ni kwa nini wanachama wa Mkataba wa Paris wanawekeza matumaini yao kwa China?

Kwanza, mikakati ya hivi karibuni ya China kuhusu hali ya hewa na nishati yanaonyesha kuwa nchi hiyo inayoongozwa na Chama cha Kikomunisti inapiga hatua kubwa katika suala hili.

Katika miongo michache yaliyopita, China imeshuhudia ukuaji wa uchumi kwa kasi pamoja na kuboreshwa kwa hali ya maisha ya raia wake. Hata hivyo, hali hii pia ilichangia madhara kwa mazingira na rasilimali. Hii ilisababisha uongozi wa China kufikiria upya kuhusu matumizi ya nishati vyenye kaboni.

"Tumeunganisha juhudi zetu za mabadiliko ya tabia nchi katika mpango wa kati na wa muda mrefu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Tunachukulia suala la kukabiliana nayo kuwa na umuhimu mkubwa, na tunajaribu kufanya maendeleo kwa kupanga njia za kisheria na kiutawala, teknolojia, na hata hali ya soko ili kuafikia ndoto hii." Rais Xi Jinping wa China alisema akihutubia wanachama kwenye Mkutano wa Paris kuhusu Mabadiliko ya tabia nchi mwaka 2015.

Hakikisho hili hasa laoneana kuchochea na kuongeza matumaini makubwa kutoka kwa jumuiya ya kisayansi kwamba China itaongoza na kukuza utawala wa kimataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Mshauri mwandamizi katika Taasisi ya Paulson inayolenga mabadiliko ya hali ya hewa Kate Gordon aliyeelezea Imani yake kwa China mara tu baada ya Trump kutangaza nia ya kuiondoa Marekani kutoka kwa mpango huo.

"Hatuna wasiwasi kuhusu uwezo wa China kuongoza ajenda hii ya hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika nishati mbadala, kupunguza  uzalishaji na matumizi ya nishati ya kaboni, na makaa ya mawe," Gordon alisema

Na yaonekana kuna uhalali kwa imani hii kwa uwezo wa China. Hii ni kwa sababu uongozi wa China unachukulia ongezeko la joto duniani kama tishio halisi.

Katika miaka michache yaliyopita, China imekuwa ikipunguza uzalishaji wa gesi chafu. Takwimu kutoka Shirika la Kimataifa la nishati la Paris zinaonyesha kwamba China imewekeza mabilioni ya dola katika vyanzo vipya vya nishati, zaidi ya Marekani na Ulaya kwa pamoja.

Na si siri kwamba miaka michache tu ya nyuma, China pamoja na Marekani na Umoja wa Ulaya yalizalisha robo moja ya kaboni duniani. Lakini China kwa kasi imepunguza uzalishaji wake wa kaboni kuliko taifa lolote lingine. Ni hivi karibuni tu ambapo taifa hilo lilisimamisha viwanda kadhaa vya makaa ya mawe vilivyokuwa vikijengwa na imekuwa ikipunguza matumizi yake ya makaa ya mawe ya kitaifa.

Jitihada za China za kiikolojia zimepewa kipaumbele katika Mpango wa Miaka Mitano ya nchi. Ili kupiga jeki ajenda hii, China tayari imewekeza rasilimali zaidi katika teknolojia za uzalishaji wa gesi isiyo na uchafuzi mkubwa, ikiwa ni pamoja na nishati ya jua, upepo, na uzalishaji wa nishati ya nyuklia.

Kuafikia viwango vya chini vya kaboni sio rahisi lakini waangalizi wanaamini kwamba China inatambua mabadiliko kutoka kwa nishati ya kaboni hadi nishati mbadala yatahakikisha maendeleo yake ya kiuchumi ya muda mrefu hasa kupitia kupatikana kwa nafasi za ajira katika viwanda vipya vya nishati mbadala

Aidha, inatia moyo kuona China imezindua mfuko wa ushirikiano wa hali ya hewa ya mabilioni ya fedha ili kutoa msaada, hasa kwa mataifa yanayoendelea kusaidia mipango yao ya hali ya hewa.

Muda wowote kuanzia sasa, mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Marekani atajulikana. Ikiwa Donald Trump ataibuka mshindi, hali ya sasa itabaki ambapo Amerika itakosa kuwa mwanachama wa Mkataba wa Paris. Lakini mgombea wa Chama cha Democratic Joe Biden anaahidi kuirejesha nchi hiyo kwenye mpango huo iwapo atachaguliwa.

Wakati wa sintofahamu hii, China iko kwenye usukani na inaonekana kuwa tayari kusukuma ushirikiano wa muungano wa kimataifa unaoibuka wenye nia ya kupambana kikamilifu na mabadiliko ya tabia nchi.

China kuongoza mapambano ya kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi

China kuongoza mapambano ya kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi