Nyambizi ya China “Fendouzhe” yatua kwenye Bonde la Mariana na kuweka rekodi mpya ya China
2020-11-10 16:57:29| cri

Nyambizi ya China “Fendouzhe” yatua kwenye Bonde la Mariana na kuweka rekodi mpya ya China

Leo asubuhi, nyambizi ya uchunguzi ya China “Fendouzhe” imetua kwa mafanikio kwenye Bonde la Mariana lenye kina cha mita 10,909 chini ya usawa wa bahari, na kuweka rekodi mpya ya China. 

“Tuko mita elfu kumi chini ya bahari, hapa kuna mandhari ya ajabu, tunatumai tunaweza kuwaonyesha wote tunayoyaona hapa kupitia video na picha zinazorekodiwa na ‘Fendouzhe’”.

Unayosikia sasa ni sauti ya baharia wa nyambizi ya “Fendouzhe” kutoka mita elfu kumi chini ya bahari. Saa 2 na dakika 12 leo asubuhi, nyambizi hiyo iliyobeba mabaharia watatu ilifanikiwa kutua salama kwenye bonde la Mariana lenye kina cha mita 10,909 chini ya usawa wa bahari.

Naibu msanifu mkuu wa nyambizi ya “Fendouzhe” Bw. Hu Zhen amesema, nyambizi hiyo kutua kwa mafanikio kwenye sehemu ya bahari yenye kina kikubwa zaidi duniani, kumethibitisha uwezo wake unaofikia vigezo vya kufanya uchunguzi wa kisayansi kwenye maeneo yote ya chini ya bahari. Anasema,

“Ugumu wake ni kuwa bonde hili ndio ni sehemu ya bahari yenye kina kirefu zaidi kote duniani, na kina hicho pia ni kikomo cha uwezo wa nyambizi yetu kama ilivyosanifiwa. Kwa hivyo safari hii ni jaribio kamili na changamoto ya pande zote kwa usanifu wetu.”

Bw. Hu Zhen ameeleza kuwa, mbali na kutua kwenye bonde la Mariana, nyambizi ya “Fendouzhe” pia itakusanya data mbalimbali za mazingira ya huko.

“Nyambizi yetu ina majukumu mawili baada ya kutua kwenye bonde la Mariana, kwanza ni kukusanya sampuli za mazingira, pili ni kusafiri kwenye eneo la chini ya bonde hilo, na kufanya uchunguzi au kupiga picha na video. Nyambizi pia hii inaweza kuchukua sampuli kwa kutumia mkono wake.”

Mtafiti wa Taasisi ya Sayansi na Uhandisi wa Chini ya Bahari iliyo chini ya Akademia ya Sayansi ya China Bw. Bao Gengsheng amesema, nyambizi hiyo pia inabeba majukumu ya kufanya utafiti wa kisayansi wa taaluma mbalimbali.

“Kwa wanajiolojia, wanaweza kuuliza kwa nini eneo hilo ndio ni sehemu ya bahari yenye kina kikubwa zaidi? Kwa wanabaiolojia, wanataka kujua kuwa katika mazingira magumu ya huko, viumbe wanaishi kivipi? Kwa wanafizikia, huenda wanataka kujua katika sehemu hii ya bahari yenye kina kikubwa zaidi duniani, mikondo ya bahari inafuata kanuni gani? Na masuala hayo yote ni masuala ya kisayansi yanayofuatiliwa zaidi na wanasayansi kwa sasa.”