Taifa la Senegal limekua la kwanza kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2022, baada ya kuibuka na ushindi wa bao moja kwa sifuri dhidi ya Guinea Bissau jana Jumapili. Mshambuliaji wa klabu ya Liverpool ya England Sadio Mane, aliifungia Senegal katika dakika ya 84 na kuikatia tiketi nchi yake ambayo mwaka 2019 ilifika hatua ya fainali na kupoteza dhidi ya Algeria. Ushindi huo wa ugenini katika mchezo huo uliochezwa jijini Bissau, umeifanya Senegal ifikishe alama 12 ambazo hazitoweza kufikiwa na timu mbili kati ya tatu zilizopo Kundi I. Kufuzu huko kwa Senegal ni mafanikio makubwa kwa kocha wao Aliou Cisse, ambaye aliwahi kuwa nahodha wa zamani wa timu hiyo kwani ameandika historia ya kuiongoza Senegal kufuzu AFCON mara mbili mfululizo.