Rais wa China atoa wito kwa nchi za BRICS kulinda kithabiti haki na usawa kimataifa
2020-11-17 20:45:02| cri

Mkutano wa 12 wa viongozi wa nchi za BRICS umefanyika leo usiku kwa njia ya video.

Akihutubia mkutano huo, Rais Xi Jinping wa China amesisitiza kuwa nchi za BRICS zinapaswa kulinda kithabiti haki na usawa duniani, kuendeleza mfumo wa pande nyingi, kulinda katiba ya Umoja wa Mataifa, kutetea mfumo wa kimataifa wenye Umoja wa Mataifa kuwa kiini chake na utaratibu wa kimataifa wenye sheria ya kimataifa kuwa msingi wake. Amesema nchi za BRICS pia zinapaswa kuwa na wazo la usalama endelevu wa pamoja, wa pande zote na wenye ushirikiano, kuondoa tofauti zao kupitia mazungumzo, kupinga vitendo vyote vya kuingilia kati mambo ya ndani ya nchi nyingine na kupinga vikwazo vya upande mmoja, ili kujenga kwa pamoja mazingira ya maendeleo yenye amani na utulivu.

Akizungumzia janga la virusi vya Corona, Rais Xi ametoa wito kwa nchi mbalimbali kuimarisha ushirikiano na mshikamano, na kuondoa tofauti na upendeleo, ili kukusanya nguvu kwenye mapambano ya pamoja dhidi ya janga hilo.