Wataalamu wa kigeni wampongeza Rais Xi Jinping kwa hotuba yake kwenye Mkutano wa 12 wa Kilele wa BRICS
2020-11-18 18:49:12| cri

Wataalamu wa kigeni wampongeza Rais Xi Jinping kwa hotuba yake kwenye Mkutano wa 12 wa Kilele wa BRICS

Mkutano wa 12 wa viongozi wa nchi za BRICS ulifanyika jana kwa njia ya video. Rais Xi Jinping wa China alihudhuria na kuhutubia mkutano huo. Wataalamu wa kigeni wamesema, hotuba ya Rais Xi imetia moyo na msukumo katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa kwenye mapambano dhidi ya janga la virusi vya Corona, kulinda kwa pamoja mfumo wa pande nyingi na kusukuma mbele ufufukaji wa uchumi wa dunia. 

Mwenyekiti wa Taasisi ya utafiti wa masuala ya kimataifa ya Uingereza ambaye ni Mbunifu wa dhana ya “Nchi za BRICS” Bw. Jim O’Neill amesema, pendekezo alilotoa Rais Xi kwenye hotuba yake la kuzitaka nchi za BRICS kulinda kithabiti haki na usawa duniani na kuendeleza mfumo wa pande nyingi, lina umuhimu mkubwa katika hali ya sasa ya kimataifa. Amesema nchi mbalimbali zinapaswa kuimarisha ushirikiano, kuharakisha utafiti wa chanjo na tiba ya virusi vya Corona, na pia kufufua uchumi kwenye msingi wa kudhibiti janga hilo. Anatarajia kuwa nchi za BRICS zitatimiza ukuaji mkubwa wa kiuchumi baada ya janga hilo.

Profesa mshiriki wa Chuo kikuu cha Urafiki wa Watu cha Russia Oleg Timofeev amesema, tangu mlipuko wa virusi vya Corona utokee, China siku zote imeshiriki kwenye ushirikiano wa kimataifa wa kupambana na virusi hivyo, kutoa uzoefu wake na msaada wa vifaa tiba kwa nchi nyingi, na uzoefu wa China unastahili kuigiwa. Amesema Russia inapenda kushirikiana na China katika kujenga utaratibu wa kimataifa wenye haki na usawa zaidi, na kutarajia kuwa nchi za BRICS zitaweka malengo mengi zaidi ya muda mrefu kwenye nyanja za ushirikiano wa pande nyingi na misaada ya kibinadamu.

Profesa wa Chuo kikuu cha Jawaharlal Nehru cha India Dk. B. R. Deepak anaona kuwa, mapendekezo ya Rais Xi kuhusu kukabiliana na janga la virusi vya Corona na kuhimiza ufufukaji wa uchumi wa dunia yanatupia macho siku za baadaye. Kwenye hotuba yake, Rais Xi alipendekeza kuhimiza ujenzi wa kituo cha utafiti wa chanjo cha nchi za BRICS, kutoa wito kwa jumuiya ya kimtaifa kutoa kipaumbele katika kuondoa umaskini, na kuharakisha ujenzi wa uhusiano wa washirika wa mapinduzi mapya ya kiviwanda kati ya nchi za BRICS, mapendekezo hayo muhimu yatakuwa nyanja zinazopewa kipaumbele kwenye ushirikiano wa nchi za BRICS.

Naye mkuu wa Chuo cha Uchumi na Biashara katika Chuo kikuu cha Witwatarsrand cha Afrika Kusini Jannie Rossouw amesema, mkutano huo uliofanyika wakati janga la virusi vya Corona bado linaendelea na nchi mbalimbali zinakabiliwa na changamoto za kiuchumi, ni muhimu sana. Amesema kuwa nguvu ya nchi moja pekee haiwezi kulishinda janga la virusi vya Corona, na inahitaji ushirikiano wa kimataifa. Anatarajia kuwa nchi za BRICS zitaimarisha ushirikiano katika udhibiti wa maambukizi, utafiti wa chanjo na ufufukaji wa uchumi wa dunia.