Afrika iko tahadhari ya wimbi la pili la COVID-19 wakati kesi zikifikia milioni 2
2020-11-19 18:24:30| cri

Nchi za Afrika ziko kwenye tahadhari kubwa ya kutokea wimbi la pili la mlipuko wa virusi vya Corona wakati idadi ya kesi za maambukizi ya virusi hivyo barani Afrika ikifikia milioni mbili.

Takwimu zilizotolewa na Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) zimeonyesha kuwa, kesi za virusi vya Corona barani Afrika zimefikia 2,013,388 mpaka kufikia leo, huku watu 48,408 wakifariki kutokana na virusi hivyo.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika Matshidiso Moeti amesema, kiwango cha upimaji wa virusi hivyo barani Afrika bado ni cha chini zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine. Amesema nchi nyingi za Afrika zinalenga kupima wasafiri, wagonjwa au watu waliokuwa karibu na wagonjwa, na huenda kesi nyingi bado hazijagunduliwa.