Uganda yaongeza ulinzi katika mji mkuu na miji mikubwa baada ya vurugu kutokea
2020-11-19 18:28:00| cri

Jeshi la Uganda limeongeza ulinzi katika mji mkuu wa nchi hiyo Kampala na miji mingine mikubwa baada ya vurugu kutokea wakati wa maandamano jana jumatano na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine 34 kujeruhiwa.

Msemaji wa jeshi hilo Brigedia Flavia Byekwaso ameliambia Shirika la Habari la China Xinhua kwa njia ya simu kuwa, askari wamepelekwa kuzuia kuongezeka kwa vurugu baada ya kukamatwa kwa mgombea urais kutoka upande wa upinzani, Robert Kyagulanyi kwa madai ya kukiuka miongozo iliyotolewa ya kudhibiti virusi vya Corona wakati wa kampeni.

Mapema mwezi huu, Tume ya Uchaguzi nchini Uganda iliwapitisha wagombea 11 wa nafasi ya urais, akiwemo rais wa sasa wa nchi hiyo Yoweri Museveni kugombea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.