RIADHA: AK yatenga Sh500,000 kwa washindi wa mbio za Mountain Running Championships
2020-11-19 16:04:35| cri

Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) limetenga jumla ya Sh500,000 kwa minajili ya kuwatuza wanariadha watakaoshiriki mbio za kitaifa za Mountain Running Championships mnamo Novemba 22, 2020 mjini Naivasha. Mratibu wa mbio hizo, Peter Angwenyi, amefichua kwamba fedha hizo za tuzo zitakuwa mahususi kwa washindi wa vitengo vya wanaume watakaoshiriki mbio za kilomita 10, wanawake watakaonogesha mbio za kilomita nane na wavulana watakaoshiriki mbio za kilomita nane. Mshindi wa kitengo cha wanaume atatia mfukoni Sh50,000, huku yule atakayeambulia nafasi ya pili akituzwa Sh25,000. Mwanariadha atakayeibuka katika nafasi ya tatu atatuzwa Sh20,000. Wengine watakaotuzwa kiasi kidogo cha fedha katika kategoria hii ni wanariadha watakaoshikilia nafasi za nne hadi 10. Mshindi wa mbio za wanawake atatia mfukoni Sh30,000 huku nambari mbili na tatu wakijizolea Sh24,000 na Sh19,000 mtawalia. Kwa mujibu wa AK, washindi wa nambari nne hadi 10 pia watatuzwa kiasi kidogo cha fedha. Mbio hizo zitakazoanza katika shule ya Cornerstone Preparatory Academy iliyoko kwenye Barabara ya Mai Mahiu – Naivasha na kumalizikia katika eneo la Flyover, zimevutia wanariadha 300.