RIADHA: Nyota wa kitaifa na kimataifa wapania kufanya makubwa NBC Marathon Dodoma
2020-11-20 16:28:00| cri

Joto la Mbio za Kimataifa za NBC Marathon zinazotarajiwa kufanyika Novemba 22 jijini Dodoma, Tanzania, limezidi kupanda baada ya washiriki kutoka ndani na nje ya nchi kuanza kuwasili katika mji huo huku wakimwaga tambo za kufanya vema. Mmoja wa wanariadha kutoka Kenya Joan Jerop Massah ametamba kufanya vema katika mbio za Kilomita 21 ‘Half Marathon’ na kuondoka na zawadi nono zilizoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC). Naye mwanariadha wa kike anayefanya vizuri katika mbio za Kilomita 42 ‘Full Marathon’ Sara Ramadhani kutoka Arusha amejinasibu kuhakikisha bendera ya Tanzania inang’ara na kukata ngebe za Wakenya. Wanariadha wengine wa Tanzania walioahidi kufanya vema ni  pamoja na Hamis Misai, Jafar Rajab kutoka Singida waliojitosa Kilomita 42.