Mwakilishi wa UNICEF nchini China atoa wito wa kufuatilia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto
2020-11-20 16:59:22| cri

Mwakilishi wa UNICEF nchini China atoa wito wa kufuatilia athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto

Novemba 20 kila mwaka ni Siku ya Watoto Duniani iliyoanzishwa na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa UNICEF kwa ajili ya kuadhimisha kupitishwa kwa Mkataba wa Haki za Watoto kwenye kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Novemba 20 mwaka 1989. Mwakilishi mkazi wa UNICEF nchini China Bibi Cynthia McCaffrey leo ametoa wito wa kufuatilia zaidi athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watoto. 

Akizungumza na Shirika Kuu la Utangazaji la China (CMG), mwakilishi wa UNICEF nchini China Bibi Cynthia McCaffrey amesema watoto wanabeba wajibu mdogo kwa mabadiliko ya tabianchi, lakini wanakabiliwa na athari kubwa kutokana na tatizo hilo. Anasema,

“Kwanza, kutokana na mabadiliko ya tabianchi, hali mbaya ya hewa kama vile dhoruba, vitaongezeka na hatimaye kuharibu maisha ya watoto. Pili, mabadiliko ya tabia ya mvua yanaathiri uzalishaji wa kilimo, na kusababisha mgogoro wa chakula. Tatu, magonjwa ya kuambukiza kama vile malaria na homa ya Dengue huwaathiri zaidi watoto wachanga na vijana. Tumegundua kuwa watoto wa chini ya miaka mitano wanakuwa wahanga wa asilimia 90 ya magonjwa yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi. Nne ni uchafuzi wa hewa. Tunakadiria kuwa watoto wapatao bilioni mbili kote duiniani wanaishi kwenye maeneo yenye kiwango cha juu cha uchafuzi wa hewa kinachozidi kigezo cha kimataifa, hali ambayo italeta athari hasi kwa ukuaji wa mwili haswa ubongo kwa watoto.”

Leo ikiwa ni siku ya watoto duniani, Bibi Cynthia McCaffrey pia ametoa mapendekezo kwa watoto na vijana wa China.

“Kwanza ni kujifunza zaidi ujuzi kuhusu mabadiliko ya tabianchi na kufahamu yanaweza kuleta athari gani kwa maisha ya watu. Pili ni kuchukua hatua, kwa mfano kutumia usafiri wa kijani, matumizi endelevu ya vitu, na kutoharibu na kutotupa chakula. Tatu ni kueneza ujuzi uliopata na hatua ulizochukua kwa wengine walio karibu nawe, na pia kwa watunga sera na watoa maamuzi.”