SOKA: Niyonzima anusurika ajali jijini Kigali
2020-11-20 16:28:24| cri

Kiungo wa klabu ya Young Africans na nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda (AMAVUBI) Haruna Fadhili Hakizimana Niyonzima, amenusurika kwenye ajali ya gari eneo Nyamata jijini Kigali. Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kuwa, Niyonzima alipata ajali hiyo alipokua akirejea jijini Kigali akitokea Wilayani  Bugesera. Ajali hiyo ilitokea jumatano wakati gari aina ya Fuso iliyokuwa ikijaribu kuipita baiskeli, na kugonga gari ya Niyonzima aliyekuwa na rafiki zake watatu. Niyonzima ambaye aliwahi kuitumikia Simba kwa miaka miwili kabla ya kurejea Young Africans mapema mwaka huu, amesema wametoka salama kwenye ajali hiyo na hakuna mtu aliyepata majeraha miongoni mwao.