Kenya na Marekani zazindua awamu ya pili ya mazungumzo ya kibiashara
2020-11-20 19:04:25| cri

Kenya na Amerika zimezindua awamu ya pili ya mazungumzo ya kibiashara, siku chache tu baada ya kinyang’anyiro cha uchaguzi nchini humo.

Amerika haijatia sahihi mikataba kama ile ya Basel na ya Paris ambayo inadhibiti usafirishaji wa taka za plastiki na udhibiti wa hali ya anga mtawalia.

Ukosefu wa Amerika kuonyesha uongozi katika mikataba hii ya kimataifa ni dhahiri kwamba watakapoenda katika mazungumzo hayo, watatumia mbinu kuwashawishi wenzao wa Kenya kulegeza misimamo yao na sheria zao kuhusiana na masuala ya kimazingira.

Nchi za kanda ya Afrika Mashariki ambazo zimekuwa zikiweka mikakati ya kuungana kiuchumi na kibiashara zimegadhabishwa sana na mashauriano hayo.

Suala la usafirishaji taka limezua tumbo joto kwa wakazi wa bara la Afrika, na kulingana na ripoti kwenye mitandao ya kijamii, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari, mazungumzo haya huenda yakadhalilisha sheria za kimazingira kama udhibiti wa plastiki ambazo Kenya na nchi zingine za Afrika zimepitisha.

Mpangilio huu unaashiria kutumia mazungumzo haya kama mbinu ya kuhakikisha kwamba kampuni hizi zinaweza kufungua soko la bidhaa hizi kwa njia tofauti.

Njia ya kwanza ni kuhakikisha kwamba Kenya inafungua uwekezaji wa viwanda hivi kwa muundo, mbinu ambayo inatoa vikwazo vilivyowekwa kuzuia bidhaa za plastiki.