Utumiaji wa mifuko ya plastiki kwa Vifungashio mwisho Desemba Tanzania
2020-11-20 19:04:01| cri

Baraza la kitaifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini Tanzania (NEMC) limeweka hadi mwishoni mwa Disemba mwaka huu kuwa mwisho ya utumiaji wa vifungashio vya chupa za maji, karanga au ubuyu.

Akizungumza na waandishi wa habari za  jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka, alisema  hivi karibuni limekuwako ongezeko la uzalishaji wa vifungashio vya plastiki ambavyo chanzo chake hakijulikani na ni vifungashio ambavyo  havina kibali cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS). 

Alisema utengenezaji, usambazani na matumizi ya vitu hivyo ni uvunjaji wa Kanuni ya 3 na 4 za Sheria ya Mazingira ya 2004, kanuni ambazo zilitungwa na kutangazwa 2019 ili kutekeleza katazo la serikali la matumizi ya plastiki.

Kanuni namba 3 inawataka wazalishaji kuwa na kibali kutoka TBS baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa, lakini hali haiko hivyo kwa sasa. Dk Gwamaka ameongeza kwamba kuwapo kwa vifungashio hivyo sokoni ni kinyume cha kanuni ya 4 (b) ambayo imetungwa na kutangazwa ili kulinda afya ya binadamu, wanyama pamoja na mazingira dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza.

Kwa mujibu wa kanuni za upigaji marufuku mifuko ya plastiki, ni marufuku kutengeneza, kuuza, kusafirisha ndani na nje ya nchi, kusambaza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote.

Dk. Gwamaka amesisitiza kuwa baraza lazima lisimamie sheria  na kuzuia matumizi ya bidhaa zisizoruhusiwa kisheria nchini humo.