WHO yaonya dhidi ya matumizi ya Remdesvir kutibu COVID-19
2020-11-20 17:08:40| cri

Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema, dawa ya Remdesvir haipaswi kutumiwa kutibu wagonjwa wa virusi vya Corona, bila kujali wana hali mbaya kiasi gani kwa kuwa hakuna ushahidi kuwa dawa hiyo inafanya kazi.

Jopo la Kundi la Mwongozo la WHO limegundua kuwa, hakuna ushahidi kuwa Remdesvir imeleta matokeo mazuri kwa wagonjwa kama kupunguza idadi ya vifo, na haja ya kuwekewa mashine ya kupumulia, na kuongeza kuwa, faida zozote za dawa hiyo kama zipo, ni ndogo sana na zinaweza kuleta madhara makubwa kwa watumiaji.

Mapendekezo ya WHO yaliyochapishwa katika jarida la Kidaktari la Uingereza, yalitokana na tathmini ya ushahidi uliohusisha takwimu kutoka majaribio manne ya kimataifa kati ya zaidi ya wagonjwa 7,000 waliolazwa hospitali.

Baada ya tathmini hiyo, Jopo hilo lilihitimisha kuwa Remdesvir haina athari kubwa katika kiwango cha vifo au matokeo mengine muhimu kwa wagonjwa.