SAKATA: FIFA yawachunguza wachezaji na maafisa mbalimbali wa Kenya katika sakata la upangaji matokeo
2020-11-24 16:53:36| cri

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeanza kuwachunguza baadhi ya wachezaji na maafisa wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Kenya ili kubaini kiwango cha kukithiri kwa matukio ya upangaji wa mechi za kipute hicho. Kitengo cha Maadili cha FIFA kimekuwa kikiendesha uchunguzi wake kuhusiana na suala hilo na kikapiga marufuku wanasoka wanne wa kikosi cha Kakamega Homeboyz baada ya kuwapata na hatia ya kupanga matokeo ya mechi mbalimbali za Ligi Kuu ya Kenya hapo awali. Katika sehemu ya uchunguzi unaoendelea kuhusu kuwepo kwa ulaghai wa upangaji wa matokeo ya mechi za Ligi Kuu ya Kenya, FIFA inaanza kuwahoji baadhi ya wanasoka na maafisa wa vikosi mbalimbali kuanzia Novemba 23, 2020. Kwa mujibu wa habari, wachezaji na maafisa wa vikosi vingi wamealikwa kwa mahojiano hayo yatakayoendeshwa na FIFA kwa wiki moja ijayo.