Maonesho ya Mwanga wa Internet yaonesha teknolojia za kisasa za akili bandia, AR na 5G
2020-11-24 17:19:54| cri

Maonesho ya Mwanga wa Internet yaonesha teknolojia za kisasa za akili bandia, AR na 5G

Maonesho ya mwanga wa Internet yakiwa ni sehemu muhimu ya mkutano wa Internet duniani unaofanyika kila mwaka mjini Wuzhen, mwaka huu kampuni zaidi ya 130 zinazoshiriki kwenye maonesho hayo zimeonesha teknolojia zao za hali ya juu, ikiwemo Akili Bandia, Cloud Computing, Big Data na 5G.

 Maonesho ya Mwanga wa Internet yaonesha teknolojia za kisasa za akili bandia, AR na 5G_fororder_e850352ac65c1038f6cfa26e722c3014b17e89aa

Mara baada ya kuingia kwenye uwanja mbele ya majumba ya maonesho hayo, utaona basi dogo linalojiendesha ambalo linatumika kusafirisha watazamaji likienda polepole uwanjani. Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa tofauti na basi la kawaida, basi hilo lenye rangi ya buluu linaloitwa Lan Pangpang, lina rada tatu za laser na kamera sita zilizowekwa kwenye kichwa chake na nyuma yake, ambazo zitalisaidia gari hilo kutambua mazingira ya karibu, na kuliwezesha kuepuka kugonga vitu na kuruhusu watu walio mbele yake kupita.

Mbali na uwezo wa kuhakikisha usalama, basi hilo pia linaweza kufuatilia hisia za abiria wake. Kwa mfano kama likigundua kuwa kuna abiria ambao hawafurahi, mfumo wake wa mawasiliano ya sauti utaanza kufanya kazi na kuwaongelesha wale wasio na furaha. Kama basi hilo likigundua kuwa abiria wake hawajisikii vizuri kiafya, litaweza kuwatambua kupitia kamera za ndani na kutoa tahadhari kwa kituo cha usimamizi, ili kutoa mwitikio wa haraka kwa hali ya dharura inayoweza kutokea.

Maonesho ya Mwanga wa Internet yaonesha teknolojia za kisasa za akili bandia, AR na 5G

Mbali na magari yanayojiendesha, kwenye maonesho hayo pia kuna kampuni nyingi zinazoonesha bidhaa zao mpya za teknolojia ya AR (Augmented Reality). Katika banda la kampuni ya Epson, baadhi ya watazamaji wanajaribu kuvaa miwani ya teknolojia ya AR, ambayo inaweza kutumika kwenye nyanja mbalimbali, kama vile burudani za nyumbani, elimu, matibabu na hata uokoaji.

Kwenye maonesho hayo, kampuni ya Huawei imeonesha teknolojia mpya ya F5G. Tofauti na mtandao wa kawaida wa 5G unaotegemea mawimbi yanayorushwa na vituo vya 5G, teknolojia ya F5G ni kama mtandao wa 5G unaounganishwa kwa mkonga wa mawasiliano wa Optic Fiber.

Imefahamika kuwa mtandao wa F5G unafaa zaidi kwa matumizi yasiyo ya kuhama kama vile kwenye maeneo ya viwanda na vituo vya kuhifadhia Data.

Hizi ni sehemu ndogo tu ya teknolojia za kisasa zinazooneshwa kwenye Maonesho haya ya Mwanga wa Internet, kwa uhakika teknolojia hizo mpya zitarahisisha zaidi kazi na maisha yetu, na kusaidia kujenga mustakbali bora wa binadamu.