Nchi 13 za Afrika zazindua majaribio ya kliniki ili kuongeza matibabu ya wagonjwa wenye dalili chache za COVID-19
2020-11-25 08:58:28| CRI

Nchi 13 za Afrika zimetangaza kuzindua ushirikiano na mashirika ya utafiti ya kimataifa ili kutekeleza majaribio ya kliniki yanayolenga kuongeza matibabu ya wagonjwa wenye dalili chache za COVID-19.

Taarifa iliyotolewa jana na Taasisi ya Madawa ya Magonjwa Yasiyofuatiliwa (DNDi) jijini Nairobi, Kenya, imesema majaribio hayo yatafanywa katika vituo 19 ili kusaidia kutambua tiba inayoweza kuzuia wagonjwa wa COVID-19 kuwa na hali mbaya.

Mashirika zaidi ya 20 ya utafiti ya kimataifa na ya Afrika yatakuwa sehemu ya Shirikisho la ANTICOV ambalo litafanya majaribio ya usalama na ufanisi wa tiba kwa wagonjwa 2,000 hadi 3,000 wa COVID-19 waliokuwa na dalili chache katika nchi 13 za Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara.

Habari nyingine zinasema, Kituo cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) kimesema, idadi ya watu walioambukizwa virusi vya Corona barani Afrika imefikia 2,080,923, huku watu 49,975 wakipoteza maisha kutokana na virusi hivyo.