Nafasi za ajira milioni 38 zapotea Afrika Mashariki kutokana na janga la COVID-19
2020-11-26 09:05:22| CRI

Soko la ajira la eneo la Afrika Mashariki limeathirika zaidi na janga la virusi vya Corona, ambapo nafasi za ajira milioni 38 zimepotea.

Hayo yamo kwenye ripoti iliyotolewa jana na Kamati ya uchumi wa Afrika ya Umoja wa Mataifa (UNECA) kuhusu athari ya virusi hivyo kwa uchumi na jamii Afrika Mashariki.

Mkuu wa Kamati hiyo, Mama Keita amesema, uchumi wa eneo hilo hautaongezeka katika mwaka 2020, isipokuwa kwa nchi nne za Tanzania, Kenya, Sudan Kusini na Ethiopia ambazo zimeonyesha ukuaji chanya wa uchumi kwa mwaka huu. Inatarajiwa kuwa uchumi nchini Sudan Kusini utakua kwa asilimia 4.1, ikifuatiwa na Tanzania na Ethiopia ambayo kila moja itapata ongezeko la karibu asilimia 2, na Kenya ongezeko la asilimia 1.  

Utabiri uliofanywa na ECA unaonyesha kuwa ongezeko la uchumi katika Afrika Mashariki litapungua sana hadi asilimia 0.6 mwaka huu kutoka asilimia 6.6 mwaka 2019.