Idadi ya watalii waliowasili nchini Kenya yaongezeka licha ya janga la COVID-19
2020-11-26 09:05:46| CRI

Mamlaka ya Takwimu nchini Kenya (KNBS) jana ilisema, licha ya janga la virusi vya Corona linaloendelea, idadi ya watalii wa kimataifa waliowasili nchini Kenya kupitia viwanja vyake viwili vikuu vya ndege vya Nairobi na Mombasa inaongezeka wakati uchumi wa dunia unafunguliwa.   

Takwimu mpya za uchumi iliyotolewa na Mamlaka hiyo huko Nairobi zinaonyesha kuwa, kuanzia mwezi Julai, idadi ya watalii waliowasili nchini Kenya iliendelea kuongezeka licha ya usumbufu unaotokana na janga la virusi vya Corona.

Ongezeko la watalii linaweka mustakabali mzuri kwa wadau wa sekta ya utalii wa nchi hiyo ambao wanategemea utalii wa ndani kujikimu kimaisha.

Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kuwa, hoteli nyingi nchini Kenya zinatarajia kuwa biashara zao zitarejea katika hali ya kawaida kabla ya mwisho wa mwaka 2021.