Ethiopia yaitaka jamii ya kimataifa kujizuia kuingilia mambo ya ndani ya nchi hiyo
2020-11-26 09:26:52| CRI

Serikali ya Ethiopia imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kujizuia kuchukua hatua zilizo kinyume na sheria na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo, wakati mapigano yakiendelea kati ya jeshi la serikali ya Ethiopia na askari wanaotii chama tawala cha Harakati za Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) kaskazini mwa nchi hiyo.

Wito huo umetolewa na waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumatano, ambapo amesisitiza haja ya kuheshimu kanuni za kutoingilia kati mambo ya ndani ya nchi.

Wakati huohuo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema, vurugu na ukosefu wa usalama zinaendelea kuenea nchini Ethiopia kutokana na watu kukimbia kutoka mji mkuu wa mkoa wa Tigray, Mekele.

Ofisi hiyo imesema, mpaka sasa, karibu watu 42,000 wamekimbilia nchini Sudan kutoka Ethiopia, watu wengine zaidi ya 95,000 wamekimbia makazi yao kusini mwa Ethiopia.