Benki ya Dunia yasema wakenya milioni 2 waingia kwenye orodha ya watu maskini wasioweza kumudu mahitaji ya kimsingi kutokana na janga la corona
2020-11-26 16:01:44| cri

Ripoti ya Benki ya Dunia ya hali ya uchumi nchini Kenya imefichua kuwa athari za kiuchumi za janga la korona zimewasukuma wakenya milioni 2 katika orodha ya watu masikini zaidi wasioweza kumudu mahitaji ya kimsingi.

Haya yamejiri wakati Kenya ikiwa mbioni kumaliza umaskini.

Hali hii imeathiri hatua ambazo serikali ya Kenya ilikuwa imepiga katika miaka mitano iliyopita, huku idadi ya watu wasio na ajira ikiendelea kuongezeka.

Ripoti hiyo iliyotolewa jana inaonyesha kuwa uchumi wa Kenya umeathirika vibaya, na inakadiria kwamba utadorora zaidi kwa asilimia moja mwaka huu.

Katika robo ya pili ya mwaka huu,uchumi wa Kenya umedorora kwa asilimia 5.7 na utahitaji kustawi kwa kiwango kikubwa ili kubadilisha hali,,jambo ambalo ni vigumu kutokea kutokana na mazingira magumu ya kiuchumi hivi sasa.

Aidha Ripoti hiyo inasema kuwa katika robo ya pili ya mwaka huu kwa kuzingatia vipimo vya ajira vya Shirika la Taifa la Takwimu (KNBS) kiwango cha ukosefu wa ajira nchini Kenya kimeongezeka hadi asilimia 10.4 .

Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa mapato ya biashara za familia yalipungua kwa takribana asilimia 50 kati ya mwezi Februari na Juni.