WHO yazitaka nchi za Afrika kuongeza utayari kwa ajili ya chanjo ya COVID-19
2020-11-27 08:55:44| CRI

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika Bi. Motshidiso Moeti amesema nchi za Afrika zinapaswa kuandaa miundombinu mipana na kuwekeza katika nguvukazi ili kuwezesha kupelekwa kwa chanjo ya virusi vya Corona katika bara hilo.

Bi. Moeti amesema, usambazaji mzuri wa chanjo ni ufunguo wa kudhibiti maambukizi ya virusi hivyo yanayoongezeka kwa kasi barani Afrika, na kuongeza kuwa, kutengeneza chanjo salama na ya uhakika ni hatua ya kwanza katika mfululizo wa kukabiliana na virusi hivyo.

Pia Bi. Moeti amesema, WHO na washirika wake wametoa miongozo ambayo serikali za nchi za Afrika zinaweza kutumia kuboresha utoaji mzuri wa chanjo ya virusi vya Corona kwa makundi yaliyo hatarini wakiwemo wazee na watu wenye magonjwa sugu.